Featured Post

HALMASHAURI KALIUA YATOA MIKOPO SHILINGI MILIONI 240

MATANGAZO

Wednesday, April 14, 2021

WAFANYABIASHARA WAONYWA KUACHA KUTOROSHA MIFUGO NJE YA NCHI!

 

Na. Edward Kondela


 

Wafanyabiashara wa mifugo nchini wametakiwa kuepuka kusafirisha mifugo yao kwenda nje ya nchi bila kufuata utaratibu kwa kuwa serikali itakosa mapato kupitia rasilimali za nchi na pia ni kosa kisheria.

 

Akizungumza jana (14.04.2021) wakati alipotembelea eneo ambalo Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepewa na Kijiji cha Horohoro Kijijini, kilichopo Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga, kwa ajili ya kuanzisha mnada wa mifugo wa mpakani, Katibu Mkuu wa wizara hiyo anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema wizara haitakuwa tayari kumtetea mfanyabiashara yeyote atakayebainika kutenda kosa hilo.

 

Prof. Gabriel amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi imedhamiria kuanzisha mnada wa mpakani kati ya Tanzania na Kenya katika Kijiji cha Horohoro Kijijini kabla ya mwaka ujao wa fedha 2021/22 ili kudhibiti baadhi ya wafanyabiashara ambao wamekuwa wakitorosha mifugo kwenda nchi ya jirani kwa ajili ya kuuza.

 

“Mfanyabiashara akibainika kufanya hivyo atashughulikiwa kwa kutumia mkono wa sheria, kwani kwa kufanya hivyo inakosesha serikali mapato kupitia rasilimali za nchi.” Amefafanua Prof. Gabriel

 

Ameongeza kuwa eneo hilo ambalo wizara imepatiwa na Kijiji cha Horohoro Kijijini lina ukubwa wa ekari 23 na lipo kando mwa barabara kuu ya kuelekea mpakani mwa Tanzania na Kenya, hivyo uwepo wa mnada huo utawezesha wafugaji wa Tanzania kuuza mifugo yao kwa wafanyabishara wa nchi hizo mbili.

 

Ametoa wito kwa wafugaji Mkoa wa Tanga na mikoa ya jirani kuwa malighafi ya biashara ya minada ni mifugo, hivyo watambue jitihada za serikali na kumnukuu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye ameitaka Sekta ya Mifugo kusogeza huduma zinazotakiwa kwa wafugaji ili mifugo yao isikonde na wafugaji wasikonde kiuchumi.

 

Aidha, amebainisha kuwa nia ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni kuhakikisha Sekta ya Mifugo inachangia zaidi katika pato la taifa hivyo ni lazima kudhibiti utoroshaji wa mifugo kwenda nchi za jirani.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Horohoro Kijijini Bw. Jumapili Yohana amesema wameamua kuipatia Wizara ya Mifugo na Uvuvi eneo hilo bila malipo yoyote wakiamini uwepo wa mnada mpakani katika kijiji hicho kutachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza ajira na kukuza biashara zingine ikiwemo ya vyakula.

 

Bw. Yohana amesema kijiji kimefuata taratibu zote za ardhi na kukubaliana kuwa mara baada ya mnada huo utakapoanza kufanya kazi utachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kijiji chao na kuishukuru wizara kwa ushirikiano.

 

Pia, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa katika ziara ya siku moja Mkoani Tanga amefika Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) na kujionea shughuli mbalimbali ikiwemo ya tafiti ya malisho bora ya mifugo na kuwaasa wafugaji kuipatia mifugo yao malisho bora ili iweze kuwa na afya njema na kuwa na nyama bora, maziwa bora na ngozi bora.

 

Amewataka wafugaji kufuga kisasa kwa kutumia sayansi na kuitaka TALIRI kusambaza tafiti zao mikoa mbalimbali ili wafugaji waweze kupata elimu ya kufuga kisasa na kuwa na mifugo bora na yenye afya ambayo itakuwa na tija kiuchumi.

 

Amewaasa pia wawekezaji na watu wanaofikiria kuwekeza, wafikirie kuwekeza katika malisho ya mifugo ili malisho bora yapatikane kwa wingi kwa kuwa wafugaji wengi wameanza kubadili fikra za ufugaji na kuhitaji malisho ya kisasa na kisayansi ambayo yanafaa kwa matokeo chanya ya mifugo yao.

 

Prof. Gabriel katika ziara yake ya siku moja Mkoani Tanga ametembelea pia Ranchi ya Mzeri iliyopo Wilaya ya Handeni na kuzungumza na wawekezaji waliopatiwa vitalu katika ranchi hiyo na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) na kukemea tabia ya baadhi ya watu wanaoiba mifugo kwenye maeneo mbalimbali nchini ikiwemo kwenye ranchi.

 

Katibu mkuu huyo pia amefika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga na kuwa na mazungumzo na mkuu wa mkoa huo Mhe. Martine Shigella pamoja na Katibu Tawala wa mkoa Bi. Judica Omari juu ya maendeleo ya sekta ya mifugo katika Mkoa wa Tanga.

 

No comments:

Post a Comment