Featured Post

HALMASHAURI KALIUA YATOA MIKOPO SHILINGI MILIONI 240

MATANGAZO

Thursday, August 13, 2020

WETCU LTD YAHAMASISHA KILIMO BORA CHA TUMBAKU TABORA


 


Na Allan Ntana, Tabora


CHAMA Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku Mkoani Tabora (WETCU LTD) kimeshika nafasi ya kwanza katika Maonesho ya Wakulima Nane Nane Kanda ya Magharibi mwaka huu na kutunukiwa cheti maalumu kwa umahiri wake wa kuhamasisha kilimo bora na kutafuta masoko ya wakulima.


Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Meneja Mkuu wa Chama hicho Samwel Jokeya alisema kuwa wao kama wasimamizi wakuu wa wakulima wa tumbaku katika eneo lao wana dhamana kubwa ya kuhakikisha zao hilo linawanufaisha wakulima.


Alisema kuwa katika maonesho ya mwaka huu walijidhatiti vya kutosha kutoa elimu stahiki kwa wakulima na kufafanua hatua kwa hatua nini wanachopaswa kufanya ili kilimo hicho kilete tija kiuchumi ikiwemo upatikanaji wa pembejeo.


Alibainisha kuwa banda lao lililopo kwenye uwanja wa maonesho hayo ya Kanda ya Magharibi lilikidhi mahitaji yote ya wakulima na lilionesha uhalisia wa shughuli zote zinazopaswa kufanywa na mkulima ili kumwongezea uzalishaji.


Jokeya aliwataka kuzingatia kanuni, taratibu na maelekezo yote waliyopewa na wataalamu na kuyafanyia kazi ili kuboresha kilimo chao na kuhakikisha kinawainuka kiuchumi.


Mwenyekiti wa Bodi ya Chama hicho Mrisho Rashid Simba alifafanua kuwa jukumu kubwa la WETCU LTD ni kuboresha shughuli za wakulima, kuhakikisha wanapata pembejeo kwa wakati na kuimarisha uhai wa vyama vya msingi.


Alitaja majukumu mengine kuwa ni kupambana na mfumuko wa masoko, kuzuia watoroshaji wa tumbaku, kutafuta makampuni (wanunuzi) wapya ambapo alibainisha kuwa juhudi zao zimewezesha kupatikana kwa wanunuzi wapya ambao ni kampuni ya Grant Tobacco Ltd (GTL), Pach-tech Ltd (PCL) na Magefa.


Ili kumaliza kero ya upatikanaji pembejeo kwa wakati alishauri makisio kufanyika mapema na mzabuni kuhakikisha anakuwa na mawakala wa usambazaji pembejeo hizo kwenye mikoa yote.


Akifafanua sababu za Kampuni hiyo kuibuka kidedea katika maonesho hayo kwa miaka 2 mfululizo kwa sekta zisizo za kiserikali, Kaimu Meneja Shughuli wa Kampuni hiyo Lazaro Abel alisema kuwa ushindi huo umechochewa na dhamira njema waliyonayo kwa wakulima.


UTAFITI TAASISI ZA KILIMO KANDA YA MAGHARIBI WAMKUNA RC ANDENGENYE

 Na Allan Ntana, Tabora


MKUU wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Msaidizi Thobias Andengenye amefurahishwa na utafiti wa mbegu za mazao unaofanywa  na taasisi za kilimo zilizoko Mikoa ya Tabora na Kigoma.


Akizungumza katika kilele cha maonesho ya wakulima nane nane Kanda ya Magharibi yaliyomalizika jana katika uwanja wa Fatma Mwassa uliopo eneo la Ipuli mjini Tabora alisema kuwa utafiti na elimu iliyotolewa na taasisi hizo imeleta tija kubwa kwa wakulima.


Alibainisha kuwa kuanzishwa kwa vituo vya utafiti wa mazao kumekuwa msaada mkubwa sana kwa wakulima kutokana na ushauri mzuri wa kitaalamu, ubunifu na dhamira njema ya kuwainua wakulima.


Andengenye alitaja taasisi ambazo zimeleta mageuzi makubwa ya sekta ya kilimo na kuanza kunufaisha wakulima kuwa ni pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Taasisi ya Utafiti wa zao la Kahawa (TACRI) na kampuni ya Felisa.


‘Tumejipanga vizuri ili kuhakikisha kilimo cha mazao ya kimkakati kinaendelea kupewa kipaumbele kikubwa katika wilaya zote za mikoa hiyo ikiwemo kuboreshwa kwa teknolojia na kusisitiza matumizi ya mbegu bora’, alisema.


Alitoa wito kwa wadau na taasisi mbalimbali hapa nchini kuja kuwekeza katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi katika Kanda hiyo ikiwemo kutoa elimu ya kilimo kwa wakulima.


Aidha alisisitiza kuendelea kuimarishwa kwa bodi za mazao na kuboreshwa kwa miradi ya ufugaji samaki katika halmashauri zote za mikoa hiyo huku akiwataka wananchi kutumia ipasavyo ujuzi na elimu waliyopata katika maonesho hayo.


Awali Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt Philemon Sengati alisema kuwa ndoto yake ni kuona maonesho ya wakulima nane nane katika Kanda hiyo yanakuwa ya mfano wa kuigwa na kanda zingine na ikiwezekana mwakani maonesho ya kitaifa yafanyikie hapo.


Aliongeza kuwa dhamira yake ni kuona maonesho ya ukanda huo yanakuwa mashamba darasa na bidhaa zote zinazoletwa ziwe na tija kubwa kwa wakulima, jamii, nchi na mataifa mengine kwa ujumla.


WAKULIMA WA TANGAWIZI BUHIGWE WAOMBA KUJENGEWA KIWANDA

 Na Allan Ntana, Tabora


WAKULIMA wa zao la tangawizi wa kijiji cha Mnzeze kata ya Mnzeze, tarafa ya Manyovu wilayani Buhigwe Mkoani Kigoma wameomba serikali kuwasaidia kutafuta wawekezaji ili kuwajengea kiwanda cha kuchakata zao hilo.


Ombi hilo limetolewa jana na wakulima wa zao hilo kutoka wilayani humo walioshiriki katika maonesho ya wakulima nane nane Kanda ya Magharibi yaliyomalizika jana katika uwanja wa Fatma Mwassa mjini Tabora.


Walisema kuwa zao hilo linalimwa kwa wingi sana katika kata hiyo yenye vijiji 4 vya Mnzeze, Kishanga, Kigogwe na Mrungu ambapo zaidi ya asilimia 90 ya wakazi wote wa kata hiyo wanalima zao hilo.


Ezekiel Joseph (46) mkulima mkazi wa kijiji hicho alisema kuwa kilimo cha zao hilo kimewanufaisha sana wananchi kwa kuwa hakina gharama kubwa na ni zao linalostahimili ukame kwa kiasi kikubwa.


Alitoa mfano wa msimu wa mwaka jana ambapo alilima ekari 2 na kufanikiwa kuvuna ya tani 16 za zao hilo ambazo zilimwezesha kupata kiasi cha sh mil 9 na kwa mwaka huu amelima jumla ya ekari 4 ambapo anatarajia kuvuna tani 32.


‘Tangawizi inastawi sana hapa Buhigwe, lakini changamoto yetu kubwa ni masoko na ukosefu wa viwanda vya kuchakata zao hilo, tunaomba serikali itusaidie kupata wawekezaji waje kutujengea kiwanda ili kuongeza thamani yake’, alisema.


Naye Amos Kayage mkulima kutoka kijiji cha Kishanga alisema kuwa zao hilo ni la biashara, hivyo kama watapata soko zuri au kiwanda watainuka sana kiuchumi na kuchangia kwa kiasi kikubwa mapato ya halmashauri yao.


Alibainisha kuwa zao la tangawizi likichakatwa kwenye mashine linaweza kutoa  mazao mengi ikiwemo unga, mbolea na mengineyo tofauti na hali ilivyo sasa, hivyo akaomba wataalamu wawape elimu zaidi ili kuboresha kilimo hicho.


Ofisa Kilimo wa halmashauri hiyo Mjairi Baraka alikiri kuwa zao hilo limewapa manufaa makubwa wakazi wa vijiji vya kata hiyo na kata jirani za Janda na Kinazi ambapo kwa wastani wanavuna hadi tani 1200 kwa mwaka ila changamoto yao kubwa ni masoko, ila juhudi za kutafuta masoko zinaendelea.


Aliongeza kuwa licha ya uhaba wa masoko kile kidogo wanachouza katika maeneo mbalimbali ikiwemo nchi jirani za Burundi, Rwanda na Kongo kimewasaidia sana kwani wengi wao wamejenga nyumba nzuri, kununua pikipiki na hata magari.