Featured Post

HALMASHAURI KALIUA YATOA MIKOPO SHILINGI MILIONI 240

MATANGAZO

Thursday, April 15, 2021

TASAF YANUFAISHA WATOTO 6,704 KIELIMU IGUNGA



 

Na Allan Ntana, Igunga

 

JUMLA ya watoto 6,704 kutoka katika familia za kaya maskini 4,766 zinazonufaika na mpango wa kunusuru kaya maskini (TASAF) wilayani Igunga Mkoani Tabora zimewezeshwa kupata elimu na mahitaji yote ya shuleni.

 

Hayo yamebainishwa jana na Mratibu Msaidizi wa TASAF wilayani humo Richard Elias Mtamani alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji mpango huo kwa waandishi wa habari waliokwenda kutembelea miradi iliyoanzishwa na kaya hizo.

 

Alisema kuwa mpango huo ulioanza kutekelezwa mwaka 2015 wilayani humo umeshanufaisha jumla ya kaya maskini 4,766 katika vijiji 54 na hadi sasa wameshawezeshwa jumla ya sh bil 5.3 na wanaendelea kupokea ruzuku hiyo.

 

Alibainisha kuwa kupitia mpango huo jumla ya watoto 6,704 kutoka katika kaya hizo wamenufaika kwa kupelekwa shule za msingi na kununuliwa mahitaji yao yote ya kielimu ikiwemo viatu, sare za shule, madaftari na kalamu.

 

Mtamani alifafanua kuwa mbali na watoto hao ambao husomeshwa katika shule za msingi na sekondari wilayani humo pia watoto 1,913 wenye umri chini ya miaka 5 wamenufaika na huduma za afya kwa kupelekwa kliniki.

 

Mtendaji wa Kijiji cha Migongwa katika kata ya Mwamashiga wilayani humo Saida Sagwa Nkuba alipongeza mpango huo wa serikali kwa kuwezesha watoto wanaotoka katika kaya maskini kupata elimu.

 

‘Hawa watoto wanafanya vizuri sana darasani, mwaka jana Suzana Daudi aliyekuwa darasa la 7 katika shule ya msingi Migongwa aliongoza kwa ufaulu katika shule zote 4 za kata hiyo na sasa anasoma Mwamashiga sekondari’, alisema.

 

Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Migongwa, Nkuba Shadi Malambo, alisema kuwa kitendo cha watoto hao kupewa mahitaji yao yote ya shule kimewahamasisha kupenda shule na kujituma katika masomo yao na sasa wanafanya vizuri sana.

 

Alieleza kuwa awali watoto hao walishindwa kuja shule kutokana na umaskini wa wazazi wao ikiwemo umbali mrefu kutoka wanakoishi hadi shuleni lakini baada ya familia zao kuanza kuwezeshwa na TASAF mahudhurio na ufaulu vimeongezeka.

 

Alitoa mfano wa matokeo ya mwaka jana ya darasa la 7 katika shule hiyo ambapo watoto 37 kati ya 43 walichaguliwa kwenda sekondari huku watoto 12 wa darasa hilo kutoka kaya maskini wakifaulu wote. 

 

Mtoto Suzane James (15) wa darasa la 6 katika shule hiyo alisema kuwa kabla ya wazazi wao kuingizwa katika mpango huo walikuwa wanashinda njaa na hawakuwa na viatu wala sare za shule jambo lililowakwamisha kuja shule.

 

No comments:

Post a Comment