Featured Post

HALMASHAURI KALIUA YATOA MIKOPO SHILINGI MILIONI 240

MATANGAZO

Wednesday, April 14, 2021

RC SENGATI AKUNWA UBORA WA MIRADI YA MAJI TABORA

 


 

Na Allan Ntana, Tabora

 

MKUU wa Mkoa wa Tabora Dkt Philemon Sengati ameleezea kufurahishwa na ubora wa miradi ya maji iliyotekelezwa na Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoani hapa katika vijijini mbalimbali.

 

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa maji safi na salama uliotekelezwa katika kijiji cha Migungumalo kata ya Usagari wilayani Uyui juzi alimpongeza Meneja wa RUWASA Mkoa kwa usimamizi bora wa miradi.

 

Alisema kuwa miradi iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali Mkoani humo imeongeza kiwango cha upatikanaji huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa vijijini kutoka asilimia 30 hadi 70.

 

‘Nimeridhishwa na utendaji wa RUWASA katika Mkoa huu, endeleeni hivi hivi, naamini miradi hii na ule wa ziwa Victoria uliogharimu zaidi ya sh bil 600 itamaliza kero ya maji katika wilaya zote 7 za mkoa wetu’, alisema.

 

Sengati alibainisha kuwa weledi na ufanisi mkubwa wa wataalamu hao umewezesha mkoa huo kuongoza nchi nzima katika utekelezaji miradi ya maji iliyogharamiwa na mradi wa P4R.

 

Alifafanua kuwa mahitaji ya maji katika mkoa huo ni lita za ujazo mil 37 wakati yaliyozalishwa kutokana na mradi mkubwa wa ziwa Victoria ni lita mil 54 hivyo kuufanya mkoa huo kuwa na maji mengi kuliko watumiaji kwa maeneo ya mjini.

 

Alieleza kuwa huduma ya maji safi na salama imeboreshwa kwa kiasi kikubwa katika mkoa huo kutokana na usimamizi bora wa miradi iliyotekelezwa hivyo akatoa wito kwa wageni kuja kujifunza kupitia miradi hiyo.

 

 

Aidha aliongeza kuwa kuboreshwa kwa huduma ya maji katika vijiji mbalimbali mkoani humo kutafanya watu wengi kuwa wasafi hivyo kuongeza kasi ya kuzaliana.

 

Sengati aliwataka wakazi wa mkoa huo kujiepusha na vitendo vya uharibifu wa mazingira ili kulinda na kutunza vyanzo vya maji vilivyopo.

 

Meneja wa RUWASA Mkoani humo Mhandisi Hatari Kapufi alisema kuwa hadi kufikia Machi 2020 wakazi 1,479,750 kati ya 2,390,039 waishio vijijini walikuwa na uwezo wa kupata huduma ya maji safi kwa asilimia 62.4 kwa baadhi ya maeneo asilimia imeongezeka hadi 70.

 

Alibainisha kuwa RUWASA imeweza kutekeleza miradi mbalimbali mkoani humo kupitia programu za PbR, P4R na Mfuko wa Maji (NWF) na hadi kufikia Machi 30 mwaka huu miradi mingi inatarajiwa kukamilika.

 

Aliongeza kuwa kupitia mpango huo jumla ya miradi 31ya maji yenye thamani ya zaidi ya sh bilioni 8.7 imetekelezwa katika mkoa huo na baadhi imekamiilka na mingine iko katika hatua za mwisho.

 

Kwa upande wake Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Kaliua Mkoani hapa Salome Luhingulanya alisema kuwa serikali ya CCM inawajali sana wananchi wake hivyo akawataka wakazi wa mkoa huo kutumia vizuri miradi hiyo.

No comments:

Post a Comment