Featured Post

HALMASHAURI KALIUA YATOA MIKOPO SHILINGI MILIONI 240

MATANGAZO

Thursday, April 15, 2021

SERIKALI YAZINDUA MRADI WA REA III (AWAMU YA 2) ....KUTUMIA SH TRIL 1.3 KUPELEKA UMEME VIJIJI VYOTE NCHINI




Na Allan Ntana, Tabora

 

SERIKALI imezindua mradi kabambe wa kusambaza Umeme Vijijini (REA Awamu ya 3 Mzunguko wa Pili ambao utafikisha nishati hiyo katika vijiji vyote ambavyo vilikuwa havijafikiwa na huduma hiyo katika mikoa na wilaya zote hapa nchini.

 

Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika jana kitaifa katika kijiji cha Ugaka kata ya Ugaka, Jimbo la Manonga wilayani Igunga Mkoani Tabora, Waziri wa Nishati Dkt Medard Matogoro Kalemani alisema kuwa mradi huo wa kipekee utatekelezwa katika vijiji, vitongoji na mitaa yote hapa nchini ndani ya miezi 18.

 

Alisema kuwa mradi huo unaofadhiliwa na serikali ya awamu ya tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia utateketekelezwa na Wakandarasi 3 kwa gharama ya zaidi ya sh tril 1.2.

 

Alibainisha kuwa hadi kufikia Desemba mwaka jana zaidi ya vijiji 10,188 kati ya  12,268 vilivyoko hapa nchini vilikuwa vimeunganishiwa nishati hiyo chini ya usimamizi wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) na sasa vimebakia vijiji 1, 974 tu ambavyo vitaunganishiwa kupitia awamu hii.

 

‘Serikali inayoongozwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli imedhamiria kufikisha umeme wa REA katika vijiji, vitongoji na mitaa yote ikiwemo taasisi za umma, hivyo akatoa wito kwa wananchi wote kuchangamkia fursa hiyo’, alisema.

 

Waziri Kalemani alifafanua kuwa tangu kuanza kwa mradi huo wa usambazaji umeme vijijini (REA) awamu ya 1, 2 na 3 hadi sasa serikali imetumia jumla ya sh tril 3.8 na kusisitiza kuwa hawataruka kijiji, kitongoji wala mtaa wowote.

Ili kutimiza lengo la serikali la kufikisha huduma hiyo katika vijiji, vitongoji na mitaa yote isiyo na umeme hapa nchini aliwataka Wakandarasi waliopewa kazi hiyo kuimaliza kwa wakati na kuonya kuwa yeyote atakayezembea atawajibishwa.

 

Aidha aliwataka Mameneja na Wataalamu wa Shirika la Umeme nchini TANESCO kufungua ofisi za muda katika vijiji vyote ili kuepusha usumbufu wa wananchi (wateja) kusafiri umbali mrefu kwenda wilayani kulipia huduma hiyo.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya REA Julius Bundala aliahidi kusimamia ipasavyo utekelezaji mradi huo ili kutimiza azma ya serikali ya kufikisha nishati hiyo katika vijiji vyote hapa nchini.

 

Katibu wa CCM Mkoa wa Tabora Solomon Kasaba alisema kuwa mradi huo ni fursa muhimu sana ya kiuchumi kwa wakazi wa vijijini hivyo akawataka kuanzisha viwanda vidogo, saluni na miradi ya uchomeleji vyuma ili kujikwamua kimaisha.

 

Naye Mkuu wa Mkoa huo Dkt Philemon Sengati alibainisha kuwa serikali imewatendea haki wakazi wa mkoa huo kwani kati ya vijiji 724 vya mkoa huo vijiji 377 vimeshaunganishiwa huduma hiyo na vilivyobaki vitapata huduma hiyo ndani ya miezi 18 tu.

 

 

No comments:

Post a Comment