Featured Post

HALMASHAURI KALIUA YATOA MIKOPO SHILINGI MILIONI 240

MATANGAZO

Tuesday, November 23, 2021

WILAYA YA KALIUA YAWAPUNGUZIA WAJAWAZITO KUJIFUNGULIA WILAYA JIRANI

 



Robert Kakwesi, Tabora

Hospitali ya Wilaya ya Kaliua,imehudumia wajawazito zaidi ya 300 katika kipindi Cha miezi kumi tangu kuanza kwake kutoa huduma.

 Katika kipindi hicho watoto zaidi ya mia tatu wamezaliwa huku wengine wakizaliwa kwa njia ya upasuaji.

 Tangu kuanzishwa kwake kuwa Wilaya mwaka 2014 ,Kaliua haikuwa na hospitali ya Wilaya baada ya kugawanywa iliyokuwa Wilaya ya Urambo na kuunda Wilaya mbili za Kaliua na Urambo.

 Kutokana na kutokuwa na hospitali yake ya Wilaya,wananchi wanaougua walikuwa wanalazimika kwenda Wilaya jirani za Uvinza,Urambo na Tabora umbali wa Hadi kufikia zaidi ya km120 na hivyo wagonjwa na wananchi kuteseka na kutumia kiasi kikubwa Cha fedha.

 Hata wajawazito nao wakilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma ya kujifungua na pale wanapolazimika kufanyiwa upasuaji Hali kuwa ngumu zaidi.

 Mganga mkuu wa halmashauri ya Wilaya ya Kaliua,Dk Lusubilo Adam,amesema wamehudumia kati ya wajawazito 300 Hadi 350 tangu waanze kutoa huduma.mwezi wa kumi mwaka Jana na kufanya zaidi ya wateja 700 kuhudumiwa wakiwemo wale wasiolazwa.

 "Mbali na kutoa huduma kwa wagonjwa na wajawazito,tumefanya upasuaji kwa wagonjwa wapatao hamsini na tunatoa huduma zilizo Bora"Amesema

 Dk Lusubilo ameongeza kuwa Wana wodi kubwa ya wajawazito inayoweza kuhudumiwa wajawazito 48 kwa wakati mmoja na kwamba dawa zipo na wataalamu wapo.

 Ameeleza kuwa wataanza kutoa huduma ya kulaza wanaume na watoto na pia huduma ya kuhifadhi maiti kwani majengo yake yamefikia hatua za mwisho kukamilika.

 Amesema kuanza kutoa huduma ya kulaza na kuhifadhi miili,kutawapunguzia gharama na muda wananchi waliokuwa wakifuata huduma wilaya jirani za Urambo na Tabora.

 Mmoja wa wanawake waliojifungua Hospitalini hapo,Zaituni Shaban,mkazi wa Ushokola,Amesema kwa kupata huduma hapo,wanaokoa fedha ambazo zinafanya shughuli zingine.

 "Tulikuwa tunapata shida ya kwenda Urambo na huko ndugu inabidi walale na kulazimika kutumia fedha nyingi tofauti na hapa"Amesema

 Mkazi wa Kazaroho,Mwanaidi Hassan,amesema mtoto wa jirani yake,alifariki baada ya kukosa huduma ya upasuaji kutokana na kukosa usafiri wa gari la kumkimbiza Wilaya Jirani ya Urambo.

 "Kama angepata usafiri Tena mapema,wangeweza kuokoa maisha yake ingawa kwa Sasa tunafurahi huduma ya upasuaji kufanyika hapa Kaliua"Amesema.

 Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Kaliua,Japhael Lufungija,amesema wameokoa muda na maisha ya watoto na wajawazito kwa kutolewa huduma wilayani Kaliua.

 Amesema baadhi ya watoto walikuwa wanapoteza maisha baada ya kuzaliwa kwa kukosa huduma muhimu ambazo hazikuwa zikitolewa kutokana na kukosekana hospitali ya Wilaya.

 Ameongeza kuwa wanaendelea kutenga bajeti ikiwa ni pamoja na kuomba Serikali Kuu ili majengo zaidi na madawa yapatikane na huduma ya mama na mtoto iwe nzuri zaidi.

 Wilaya ya Kaliua iliyoanzishwa mwaka 2014,haikuwa na Hospitali ya Wilaya na wakazi wake zaidi ya laki tatu,kutegemea huduma wilaya ya Urambo na Tabora umbali zaidi ya km 120.