Featured Post

HALMASHAURI KALIUA YATOA MIKOPO SHILINGI MILIONI 240

MATANGAZO

Friday, September 4, 2020

ATHARI ZA WATOTO KIMAKUZI AMBAO MAMA ZAO WAMEFUNGWA GEREZANI AU WAPO MAHABUSU

 MWANAIDI Ramdhani(jina sio lake) alikaa mahabusu kwa miezi tisa akituhumiwa kuua pasipo kukusudia ,hawara wa mzazi mwenzake waliyezaa naye watoto wawili. 

 Mwanaidi baadae alitiwa hatiani na Mahakama kuu kwa kosa la kuua pasipo kukusudia na kuhukumiwa kifungo cha miaka saba jela. 

 Akiwa na mtoto wake wa miezi sita,alilazimika kuishi naye mahabusu na baadae Gerezani alipoanza kutumikia kifungo chake,mtoto akiwa na miaka miwili angali bado akinyonya. 

Akiishi kijiji cha Nkokoto,kata ya Vumilia wilayani Urambo,Mwanaidi anasema alikutana na masahibu ya kumuua hawara wa mzazi mwenzie baada ya kuwafumania wakiwa katika nyumba ya rafiki ya mzazi mwenzie.(anamtaja jina) 

 Anasema chanzo cha tukio hilo ni baada ya kuelezwa na mmoja wa shoga zake kuwa mzazi mwenzie anamsaliti kwa kuwa na hawara ambaye wanakutana kwenye chumba cha rafiki yake mzazi mwenzie.. 

"Nilijawa hasira na kwa kweli nilipowakuta,mzazi mwenzangu alikimbia nami sikuwa namhitaji muda huo bali mwenzie ambaye alibaki akishangaa nami kumpiga na kiti nilichokikuta chumbani kwenye kichwa chake'Anasema na kuangua kilio. 

 Kwa kweli ni simulizi ambayo ilikuwa ngumu kuelezwa kwa vile hapendi kukumbuka tukio hilo lililotokea miaka tisa iliyopita ambalo limesambaratisha maisha yake hadi leo amekuwa mtu wa kuhama kutoka kwa ndugu mmoja kwenda kwa mwingine.

 Mwanaidi anasema tukio hilo,lilimfanya apoteze mwanae wa kwanza aliyemzaa na mzazi mwenzie miaka miwili baada ya kutumikia kifungo gerezani huku mzazi mwenzie akikimbia kusikojulikana na hana mawasiliano naye. 

 Lakini hilo sio lengo kumuuliza bali kutaka kufahamu maisha aliyoishi mahabusu na gerezani wakati ametiwa mikononi mwa vyombo vya Dola. 

 "Moja ya adha niliyoipata ni uwezo wa kushindwa kumnyonyesha mwanangu inavyotakiwa kwani maziwa yalikuwa tabu kutoka na yakitoka ni kidogo kwa mtoto kushiba hivyo muda mwingi alikuwa akilia"Anasema  akiwa mahabusu gereza la mahabusu Tabora maarufu kwa jina la kwa Zubery,alikuwa akiishi na mwanae na kuwa na wakati mgumu kuhimili mazingira ya sehemu hiyo akiwa na mtoto mdogo wa miezi sita. 

 Mwanaidi naye anaungana na Mariam Daud(naye sio jina lake) ambaye alitumikia gerezani miaka saba baada ya kukutwa  na  hatia  ya kumuua pasipo kukusudia,mke mwenzie kutokana na wivu wa kimapenzi.  

Mariam  anadai wakati ananyoneyesha mtoto wake wa miezi miwili,mumewe hakuwa anamjali bali kuhamishia penzi kwa mke mwenzake na ndipo ulipotokea ugomvi baina yake na mke mwenzie na kumpiga na kigoda kichwani na kusababisha kifo chake. 

 Naye anaeleza adha kubwa aliyoipata mahabusu na gerezani kwa kuishi na mwanae mdogo na kulalamika maziwa yake kuwa kidogo tofauti na alipokuwa nyumbani. 

 Wanawake wote wawili wanaeleza mazingira magumu kwa watoto wao wadogo ambao walilazimika kuwa magerezani au mahabusu baada ya kufanya makossa ya jinai. 

 Wanwake hao wanawakilishi wengine kadhaa ambao wanatumikia kifungo wakiwa na watoto wanaowanyonyesha. 

 Daktari wa watoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora,Kitete,Dk Mnubi Baguma,anasema kuwa athari kubwa kwa watoto wanaolelewa katika mazingira yasiyo rafiki kwao yakiwemo magereza na mahabusu. 

 Anasema mtoto kwanza hatopata maziwa ya kutosha kutoka kwa mama yake kutokana na msongo wa mawazo aliyonayo baada ya tukio lakini pia na mazingira mapya anayoishi ambayo hakuyatarajia. 

“Maziwa ya mama pia hutegemea saikolojia yake achilia mbali chakula anachokula” Anaeleza kuwa kwa mazingira anayokuwepo mzazi akiwa na mtoto anayenyonya,atalazimika kupata maziwa ya ziada ya kopo kwa vile ya mama hayatamtosha na hilo anasema sio jambo la kufurahia,akisisitiza kuwa mtoto anapaswa kunyonya maziwa ya mama pekee kwa muda wa miezi sita mfululizo bila kupewa kitu kingine chochote yakiwemo hata maji. 

 “Maziwa ya mama kwa kipindi hicho yanatengenezwa kwa namna yake kiasi kwamba mahitaji yote ya mtoto yapo yakiwemo maji”Anasema Dk baguma anaeleza kwamba baada ya miezi sita ndio mtoto anaweza kuanza kupewa vyakula vingine huku akiendelea kunyonya hadi anafikisha miaka miwili au mitatu kutegemea hali yake. 

 Anasema wanawake wanaopata bahati mbaya ya kufungwa au kuwa mahabusu wakiwa na watoto wanaowanyonyesha,athari zao ni mbaya katika makuzi yao kwa vile wanakosa msingi mzuri na muhimu wa maisha yao. 

 Anaeleza kwamba mtoto huanza kujengwa tangu mimba inapoingia ambayo ni msingi mkuu wa maisha yake,yanayoendelea pale mimba inapokua kisha kuzaliwa hadi anafikisha miaka mitatu hadi mitano. 

 “Msingi mkubwa wa mtoto kimakuzi na kiakili huanza kujengwa mimba inapotungwa,kulelewa hadi kuzaliwa na kuendelea wakati akinyonya mpaka anapoacha kunyonya”

Anasema Ni Dhahiri kuwa msingi wa makuzi ya akili ya mtoto anayeishi mahabusu au gerezani na mzazi wake unakuwa haupo vizuri,ambapo hupata msingi mbaya wa maisha yake. 

 Dk Baguma anasema mtoto anahitaji kucheza katika ukuaji wake na hivyo kuimarisha afya yake ya mwili na akili jambo linalokuwa tofauti kwa mtoto aliye gerezani au mahabusu,ambaye afya yake na akili inaathirika. 

 Anasisistiza kuwa akili ya mtoto humuathiri hata akikua na kuanza shule kwani anakua hajiamini na kujitenga sababu anakuwa anajengwa na kuathirika akiwa tumboni au baada ya kuzaliwa,akiongeza kuwa mara nyingi huathirika hadi utu uzima wake. 

 Mtaalamu wa elimu ya malezi kwa makuzi ya mtoto,afisa muuguzi katika zahanati ya Mjini Tabora,Catherine Mushi,anasema elimu hiyo ni muhimu kwa vile inamsaidia kukua kimwili,kiakili,kihisia na kijamii.anaeleza kuwa elimu hiyo huanzia tangu ujauzito hadi umri wa miaka mitatu. 

 Anasema watoto hupenda kusikia sauti mbalimbali na ndio maana hugonga vitu kama makopo,masufuria n.k kitendo kinachojenga akili yake jambo ambalo mtoto aliye mahabusu au gerezani akiwa na mzazi wake analikosa. 

 Mushi anabainisha kuwa mtoto anajifunza kutambua rangi na vitu mbalimbali,akisisitiza elimu ya utambuzi huanzia nyumbani na sio sehemu nyingine yoyote,jambo linalodhihirisha watoto walio mahabusu au gerezani hukosa fursa hiyo muhimu. 

 Anabainisha kuwa pamoja na wazazi kutakiwa kuzungumza na watoto wao wangali tumboni na baada ya kuzaliwa,bado wanahitajika kucheza nao michezo mbalimbali na kuwaimbia. 

 “Katika kucheza na mtoto na kumpa fursa ya kushika vitu mbalimbali,kunakomaza misuli ya mtoto”Anasema Mushi anasema watoto hufuatilia na kujifunza hata kama hawezi kuzungumza,akieleza huweka msingi imara wa kujifunza hata wakati wa kuzungumza naye jambo linalomfanya aanze kutambua na kutofautisha sauti za watu akiwemo mama yake. 

 Ni wazi kuwa kwa mama mwenye msongo wa mawazo anayeugua ugonjwa wa sonona,kutokana na madhila aliyopata,hawezi kufanya hayo kwa mtoto kutokana na hali yake na mazingira na hivyo kumkosesha msingi mzuri wa makuzi yake. 

 Mushi anabainisha kuwa tafiti za watoto zinaonesha wale waliopewa msingi bora wa malezi kuanzia utungwaji mimba,inapolelewa hadi anapotimiza miaka mitatu,kuwa tabia zao nzuri hazibadiliki hata wakiwa wakubwa. 

 Kwa watoto wanaoishi na wazazi wao magerezani au mahabusu,anasema ni Dhahiri wana shida kubwa kwa wao kukosa mambo ya msingi katika makuzi yao. 

 Mwanasheria wa asasi isiyo ya Kiserikali ya Jamii Salama Development Volunteer,JSDV,ambayo inajishughulisha na utoaji elimu ya sheria kwa wasaidizi wa kisheria,Paralegal,Charles Ayo,anasema sheria ya mtoto ya mwaka 2009 inakataza mtoto kutwezwa au kushushwa utu wake. 

 Anasema mtoto ambaye mzazi wake anatumikia kifungo na yeye kulazimika kuwa naye gerezani au mahabusu,anakuwa anatwezwa utu wake kwani anakosa uhuru wa kutopata haki zake kama mtoto,ikiwemo kucheza na kushiriki na wenzake huku pia akiwa katika mazingira ya adhabu. 

“Mazingira ya gerezani au mahabusu sio huru kwani yanajulikana huku mtoto akiwekwa mbali na jamii”Anasema Ayo anabainisha kuwa moja ya sababu ya mtoto kuishi na mama yake gerezani au mahabusu ni kupata haki yake ya kunyonya ,lakini mazingira hayafai kwake na yeye sio mtenda kosa. 

Anasisitiza kuwa ni vema mtoto akawekwa katika mazingira mazuri na salama kwake tofauti na ilivyo sasa. 

 Makamu mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika,TLS,kanda ya Tabora,Kanani Chombala,anasema mama hawezi kupewa msamaha sababu ya kuwa na mtoto na kuiomba Serikali kuangalia maslahi mapana ya mtoto. 

 Chombala anaungana na wengine kubainisha kuwa chakula cha gerezani sio kizuri na ni cha aina moja huku akisema mzazi anapata adhabu mara mbili ya kufungwa na mtoto wake kuwa mazingira yasiyostahili na kuteseka. 

 Mkataba wa kimataifa wa watoto (CRC) wa mwaka 1989,unataka watoto kuanzia ujauzito hadi wafikishapo miaka mitatu kupata lishe bora, ulinzi na mahitaji bora kwa ajili ya makuzi yao na kuimarisha ubongo. 

 Ni dhahiri kwamba kwa watoto wanaokulia gerezani na wazazi wao hawayapati kwa vile hakuna lishe bora wanayopata wazazi wao na hivyo hawanyonyi maziwa bora kutoka kwa wazazi. Kwa kukulia kwao gerezani au magerezani, watoto wanakosa muda na haki ya kucheza mambo ambayo ni muhimu kwa maisha yao. 

 Watoto kukulia gerezani athari zake wanaishi mazingira yasiyo rafiki kwao huku wakipata adhabu ambazo hawazistahili, kwani mazingira ya kuishi na kulala sio rafiki kwao na hivyo kuathirika kiafya na kiakili wakiwa wadogo na hata wakikua.