Featured Post

HALMASHAURI KALIUA YATOA MIKOPO SHILINGI MILIONI 240

MATANGAZO

Wednesday, April 21, 2021

TUNAOMBA MSAADA WA UJENZI WA MSIKITI

WAISLAM TABORA WAOMBA MSAADA.

Waislam katika msikiti wa Ijumaa Ikindwa kata ya Kiloleni Manispaa ya Tabora wameshindwa kukamilisha ujenzi wa msikiti huo kwa kile kinachoelezwa kukosa uwezo wa kifedha wa kumalizia msikiti huo ambao unahitaji zaidi ya shilingi million tano.

Sunday, April 18, 2021

PROF. GABRIEL AAGIZA UZALISHAJI WA CHANJO YA UGONJWA WA MIGUU NA MIDOMO MWAKANI!

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza na baraza la wafanyakazi la Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) jijini Dar es Salaam na kuitaka TVLA kuhakikisha mwaka ujao inazalisha chanjo ya mifugo ya ugonjwa wa miguu na midomo (FMD) ili bidhaa zitokanazo na mifugo ziweze kupata masoko ya kimataifa. (Picha na Edward Kondela)

 


Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Hezron Nonga akizungumza na baraza la wafanyakazi la Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) jijini Dar es Salaam (hawapo pichani) na kukiarifu kikao hicho kuwa mkakati uliopo ni kuhakikisha mwaka ujao zinazalishwa chanjo tatu za mifugo ikiwemo ya kichaa cha mbwa ili kufikia ukomo wa ugonjwa huo. (Picha na Edward Kondela)

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Stella Bitanyi akizungumza kwenye baraza la wafanyakazi la TVLA na kubainisha kuwa tayari wamezalisha chanjo ya saba ya homa ya mapafu ya mbuzi kati ya chanjo 13 za kimkakati na imethibtishwa na maabara ya chanjo za mifugo Afrika na imepata cheti cha ubora na uzalishaji wake umeshaanza. (Picha na Edward Kondela)

 


Wajumbe wa baraza la wafanyakazi la Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) wakisikiliza hoja mbalimbali kutoka kwa viongozi wao (hawapo pichani) akiwemo mgeni rasmi aliyefungua kikao cha baraza hilo Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel. Kikao kimefanyika katika ukumbi wa TVLA jijini Dar es Salaam. (Picha na Edward Kondela)

Picha ya pamoja ya mgeni rasmi Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel baada ya kufungua kikao cha baraza la wafanyakazi la Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) jijini Dar es salaam. (Picha na Edward Kondela)

  


 Na. Edward Kondela

 

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel ameagiza upatikanaji wa chanjo ya mifugo ya ugonjwa wa miguu na midomo (FMD) ifikapo mwakani ili bidhaa zitokanazo na mifugo ziweze kuuzwa katika masoko ya kimataifa.

Prof. Gabriel ameyasema hayo jana (16.04.2021) jijini Dar es Salaam wakati akifungua kikao cha baraza la wafanyakazi la Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), ambapo amemuelekeza Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Prof. Hezron Nonga kusimamia utekelezaji wa uanzishwaji wa chanjo hiyo ili kuwezesha viwanda vinavyozalisha nyama zitokanazo na mifugo hapa nchini kupata masoko ya bidhaa zao katika nchi mbalimbali.

Aidha ameitaka TVLA kuhakikisha changamoto ya homa ya nguruwe inatatuliwa kwa kupatikana kwa chanjo yake na kutokomeza kabisa ugonjwa huo hapa nchini na kuondoa dhana iliyojengeka kwa baadhi ya wananchi kuwa baadhi ya mifugo imekuwa ikibaguliwa katika upatikanaji wa huduma mbalimbali zikiwemo za chanjo. 

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Hezron Nonga amesema mkakati uliopo ni kuhakikisha mwaka ujao zinazalishwa chanjo tatu za mifugo ikiwemo ya kichaa cha mbwa ili kufikia ukomo wa ugonjwa huo kwa kuwa lengo la dunia ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 ugonjwa huo unatokomezwa duniani.

Pia amesema chanjo zingine za ugonjwa wa sotoka ya mbuzi na kondoo tayari hatua zaidi zinaendelea kufanywa na TVLA ili kuhakikisha mwaka ujao chanjo hizo zinazalishwa hapa nchini pamoja na kuzalisha chanjo ya mapele ngozi. 

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Stella Bitanyi amesema wakala hiyo tayari imezalisha chanjo ya saba ya homa ya mapafu ya mbuzi kati ya chanjo 13 za kimkakati na tayari imethibtishwa na maabara ya chanjo za mifugo Afrika na imepata cheti cha ubora na uzalishaji wake umeshaanza. 

Dkt. Bitanyi amesema TVLA inatategemea kuzindua chanjo hiyo kati ya Mwezi Mei na Juni mwaka huu ili itangazwe na wafugaji waanze kuitumia pamoja na kuweka mikakati ya uwezo wa kuzalisha zaidi chanjo dhidi ya homa ya mapafu ya ng’ombe kwa kuagiza mashine yenye uwezo mkubwa zaidi wa kuzalisha chanjo hiyo.

Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) ambayo ipo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi inafanya jitihada mbalimbali kuhakikisha inazalisha chanjo 13 za mifugo ambazo ni za kimkakati.

Thursday, April 15, 2021

TASAF YANUFAISHA WATOTO 6,704 KIELIMU IGUNGA



 

Na Allan Ntana, Igunga

 

JUMLA ya watoto 6,704 kutoka katika familia za kaya maskini 4,766 zinazonufaika na mpango wa kunusuru kaya maskini (TASAF) wilayani Igunga Mkoani Tabora zimewezeshwa kupata elimu na mahitaji yote ya shuleni.

 

Hayo yamebainishwa jana na Mratibu Msaidizi wa TASAF wilayani humo Richard Elias Mtamani alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji mpango huo kwa waandishi wa habari waliokwenda kutembelea miradi iliyoanzishwa na kaya hizo.

 

Alisema kuwa mpango huo ulioanza kutekelezwa mwaka 2015 wilayani humo umeshanufaisha jumla ya kaya maskini 4,766 katika vijiji 54 na hadi sasa wameshawezeshwa jumla ya sh bil 5.3 na wanaendelea kupokea ruzuku hiyo.

 

Alibainisha kuwa kupitia mpango huo jumla ya watoto 6,704 kutoka katika kaya hizo wamenufaika kwa kupelekwa shule za msingi na kununuliwa mahitaji yao yote ya kielimu ikiwemo viatu, sare za shule, madaftari na kalamu.

 

Mtamani alifafanua kuwa mbali na watoto hao ambao husomeshwa katika shule za msingi na sekondari wilayani humo pia watoto 1,913 wenye umri chini ya miaka 5 wamenufaika na huduma za afya kwa kupelekwa kliniki.

 

Mtendaji wa Kijiji cha Migongwa katika kata ya Mwamashiga wilayani humo Saida Sagwa Nkuba alipongeza mpango huo wa serikali kwa kuwezesha watoto wanaotoka katika kaya maskini kupata elimu.

 

‘Hawa watoto wanafanya vizuri sana darasani, mwaka jana Suzana Daudi aliyekuwa darasa la 7 katika shule ya msingi Migongwa aliongoza kwa ufaulu katika shule zote 4 za kata hiyo na sasa anasoma Mwamashiga sekondari’, alisema.

 

Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Migongwa, Nkuba Shadi Malambo, alisema kuwa kitendo cha watoto hao kupewa mahitaji yao yote ya shule kimewahamasisha kupenda shule na kujituma katika masomo yao na sasa wanafanya vizuri sana.

 

Alieleza kuwa awali watoto hao walishindwa kuja shule kutokana na umaskini wa wazazi wao ikiwemo umbali mrefu kutoka wanakoishi hadi shuleni lakini baada ya familia zao kuanza kuwezeshwa na TASAF mahudhurio na ufaulu vimeongezeka.

 

Alitoa mfano wa matokeo ya mwaka jana ya darasa la 7 katika shule hiyo ambapo watoto 37 kati ya 43 walichaguliwa kwenda sekondari huku watoto 12 wa darasa hilo kutoka kaya maskini wakifaulu wote. 

 

Mtoto Suzane James (15) wa darasa la 6 katika shule hiyo alisema kuwa kabla ya wazazi wao kuingizwa katika mpango huo walikuwa wanashinda njaa na hawakuwa na viatu wala sare za shule jambo lililowakwamisha kuja shule.

 

SERIKALI YAZINDUA MRADI WA REA III (AWAMU YA 2) ....KUTUMIA SH TRIL 1.3 KUPELEKA UMEME VIJIJI VYOTE NCHINI




Na Allan Ntana, Tabora

 

SERIKALI imezindua mradi kabambe wa kusambaza Umeme Vijijini (REA Awamu ya 3 Mzunguko wa Pili ambao utafikisha nishati hiyo katika vijiji vyote ambavyo vilikuwa havijafikiwa na huduma hiyo katika mikoa na wilaya zote hapa nchini.

 

Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika jana kitaifa katika kijiji cha Ugaka kata ya Ugaka, Jimbo la Manonga wilayani Igunga Mkoani Tabora, Waziri wa Nishati Dkt Medard Matogoro Kalemani alisema kuwa mradi huo wa kipekee utatekelezwa katika vijiji, vitongoji na mitaa yote hapa nchini ndani ya miezi 18.

 

Alisema kuwa mradi huo unaofadhiliwa na serikali ya awamu ya tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia utateketekelezwa na Wakandarasi 3 kwa gharama ya zaidi ya sh tril 1.2.

 

Alibainisha kuwa hadi kufikia Desemba mwaka jana zaidi ya vijiji 10,188 kati ya  12,268 vilivyoko hapa nchini vilikuwa vimeunganishiwa nishati hiyo chini ya usimamizi wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) na sasa vimebakia vijiji 1, 974 tu ambavyo vitaunganishiwa kupitia awamu hii.

 

‘Serikali inayoongozwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli imedhamiria kufikisha umeme wa REA katika vijiji, vitongoji na mitaa yote ikiwemo taasisi za umma, hivyo akatoa wito kwa wananchi wote kuchangamkia fursa hiyo’, alisema.

 

Waziri Kalemani alifafanua kuwa tangu kuanza kwa mradi huo wa usambazaji umeme vijijini (REA) awamu ya 1, 2 na 3 hadi sasa serikali imetumia jumla ya sh tril 3.8 na kusisitiza kuwa hawataruka kijiji, kitongoji wala mtaa wowote.

Ili kutimiza lengo la serikali la kufikisha huduma hiyo katika vijiji, vitongoji na mitaa yote isiyo na umeme hapa nchini aliwataka Wakandarasi waliopewa kazi hiyo kuimaliza kwa wakati na kuonya kuwa yeyote atakayezembea atawajibishwa.

 

Aidha aliwataka Mameneja na Wataalamu wa Shirika la Umeme nchini TANESCO kufungua ofisi za muda katika vijiji vyote ili kuepusha usumbufu wa wananchi (wateja) kusafiri umbali mrefu kwenda wilayani kulipia huduma hiyo.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya REA Julius Bundala aliahidi kusimamia ipasavyo utekelezaji mradi huo ili kutimiza azma ya serikali ya kufikisha nishati hiyo katika vijiji vyote hapa nchini.

 

Katibu wa CCM Mkoa wa Tabora Solomon Kasaba alisema kuwa mradi huo ni fursa muhimu sana ya kiuchumi kwa wakazi wa vijijini hivyo akawataka kuanzisha viwanda vidogo, saluni na miradi ya uchomeleji vyuma ili kujikwamua kimaisha.

 

Naye Mkuu wa Mkoa huo Dkt Philemon Sengati alibainisha kuwa serikali imewatendea haki wakazi wa mkoa huo kwani kati ya vijiji 724 vya mkoa huo vijiji 377 vimeshaunganishiwa huduma hiyo na vilivyobaki vitapata huduma hiyo ndani ya miezi 18 tu.

 

 

Wednesday, April 14, 2021

WAFANYABIASHARA WAONYWA KUACHA KUTOROSHA MIFUGO NJE YA NCHI!

 

Na. Edward Kondela


 

Wafanyabiashara wa mifugo nchini wametakiwa kuepuka kusafirisha mifugo yao kwenda nje ya nchi bila kufuata utaratibu kwa kuwa serikali itakosa mapato kupitia rasilimali za nchi na pia ni kosa kisheria.

 

Akizungumza jana (14.04.2021) wakati alipotembelea eneo ambalo Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepewa na Kijiji cha Horohoro Kijijini, kilichopo Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga, kwa ajili ya kuanzisha mnada wa mifugo wa mpakani, Katibu Mkuu wa wizara hiyo anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema wizara haitakuwa tayari kumtetea mfanyabiashara yeyote atakayebainika kutenda kosa hilo.

 

Prof. Gabriel amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi imedhamiria kuanzisha mnada wa mpakani kati ya Tanzania na Kenya katika Kijiji cha Horohoro Kijijini kabla ya mwaka ujao wa fedha 2021/22 ili kudhibiti baadhi ya wafanyabiashara ambao wamekuwa wakitorosha mifugo kwenda nchi ya jirani kwa ajili ya kuuza.

 

“Mfanyabiashara akibainika kufanya hivyo atashughulikiwa kwa kutumia mkono wa sheria, kwani kwa kufanya hivyo inakosesha serikali mapato kupitia rasilimali za nchi.” Amefafanua Prof. Gabriel

 

Ameongeza kuwa eneo hilo ambalo wizara imepatiwa na Kijiji cha Horohoro Kijijini lina ukubwa wa ekari 23 na lipo kando mwa barabara kuu ya kuelekea mpakani mwa Tanzania na Kenya, hivyo uwepo wa mnada huo utawezesha wafugaji wa Tanzania kuuza mifugo yao kwa wafanyabishara wa nchi hizo mbili.

 

Ametoa wito kwa wafugaji Mkoa wa Tanga na mikoa ya jirani kuwa malighafi ya biashara ya minada ni mifugo, hivyo watambue jitihada za serikali na kumnukuu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye ameitaka Sekta ya Mifugo kusogeza huduma zinazotakiwa kwa wafugaji ili mifugo yao isikonde na wafugaji wasikonde kiuchumi.

 

Aidha, amebainisha kuwa nia ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni kuhakikisha Sekta ya Mifugo inachangia zaidi katika pato la taifa hivyo ni lazima kudhibiti utoroshaji wa mifugo kwenda nchi za jirani.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Horohoro Kijijini Bw. Jumapili Yohana amesema wameamua kuipatia Wizara ya Mifugo na Uvuvi eneo hilo bila malipo yoyote wakiamini uwepo wa mnada mpakani katika kijiji hicho kutachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza ajira na kukuza biashara zingine ikiwemo ya vyakula.

 

Bw. Yohana amesema kijiji kimefuata taratibu zote za ardhi na kukubaliana kuwa mara baada ya mnada huo utakapoanza kufanya kazi utachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kijiji chao na kuishukuru wizara kwa ushirikiano.

 

Pia, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa katika ziara ya siku moja Mkoani Tanga amefika Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) na kujionea shughuli mbalimbali ikiwemo ya tafiti ya malisho bora ya mifugo na kuwaasa wafugaji kuipatia mifugo yao malisho bora ili iweze kuwa na afya njema na kuwa na nyama bora, maziwa bora na ngozi bora.

 

Amewataka wafugaji kufuga kisasa kwa kutumia sayansi na kuitaka TALIRI kusambaza tafiti zao mikoa mbalimbali ili wafugaji waweze kupata elimu ya kufuga kisasa na kuwa na mifugo bora na yenye afya ambayo itakuwa na tija kiuchumi.

 

Amewaasa pia wawekezaji na watu wanaofikiria kuwekeza, wafikirie kuwekeza katika malisho ya mifugo ili malisho bora yapatikane kwa wingi kwa kuwa wafugaji wengi wameanza kubadili fikra za ufugaji na kuhitaji malisho ya kisasa na kisayansi ambayo yanafaa kwa matokeo chanya ya mifugo yao.

 

Prof. Gabriel katika ziara yake ya siku moja Mkoani Tanga ametembelea pia Ranchi ya Mzeri iliyopo Wilaya ya Handeni na kuzungumza na wawekezaji waliopatiwa vitalu katika ranchi hiyo na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) na kukemea tabia ya baadhi ya watu wanaoiba mifugo kwenye maeneo mbalimbali nchini ikiwemo kwenye ranchi.

 

Katibu mkuu huyo pia amefika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga na kuwa na mazungumzo na mkuu wa mkoa huo Mhe. Martine Shigella pamoja na Katibu Tawala wa mkoa Bi. Judica Omari juu ya maendeleo ya sekta ya mifugo katika Mkoa wa Tanga.

 

RC SENGATI AKUNWA UBORA WA MIRADI YA MAJI TABORA

 


 

Na Allan Ntana, Tabora

 

MKUU wa Mkoa wa Tabora Dkt Philemon Sengati ameleezea kufurahishwa na ubora wa miradi ya maji iliyotekelezwa na Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoani hapa katika vijijini mbalimbali.

 

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa maji safi na salama uliotekelezwa katika kijiji cha Migungumalo kata ya Usagari wilayani Uyui juzi alimpongeza Meneja wa RUWASA Mkoa kwa usimamizi bora wa miradi.

 

Alisema kuwa miradi iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali Mkoani humo imeongeza kiwango cha upatikanaji huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa vijijini kutoka asilimia 30 hadi 70.

 

‘Nimeridhishwa na utendaji wa RUWASA katika Mkoa huu, endeleeni hivi hivi, naamini miradi hii na ule wa ziwa Victoria uliogharimu zaidi ya sh bil 600 itamaliza kero ya maji katika wilaya zote 7 za mkoa wetu’, alisema.

 

Sengati alibainisha kuwa weledi na ufanisi mkubwa wa wataalamu hao umewezesha mkoa huo kuongoza nchi nzima katika utekelezaji miradi ya maji iliyogharamiwa na mradi wa P4R.

 

Alifafanua kuwa mahitaji ya maji katika mkoa huo ni lita za ujazo mil 37 wakati yaliyozalishwa kutokana na mradi mkubwa wa ziwa Victoria ni lita mil 54 hivyo kuufanya mkoa huo kuwa na maji mengi kuliko watumiaji kwa maeneo ya mjini.

 

Alieleza kuwa huduma ya maji safi na salama imeboreshwa kwa kiasi kikubwa katika mkoa huo kutokana na usimamizi bora wa miradi iliyotekelezwa hivyo akatoa wito kwa wageni kuja kujifunza kupitia miradi hiyo.

 

 

Aidha aliongeza kuwa kuboreshwa kwa huduma ya maji katika vijiji mbalimbali mkoani humo kutafanya watu wengi kuwa wasafi hivyo kuongeza kasi ya kuzaliana.

 

Sengati aliwataka wakazi wa mkoa huo kujiepusha na vitendo vya uharibifu wa mazingira ili kulinda na kutunza vyanzo vya maji vilivyopo.

 

Meneja wa RUWASA Mkoani humo Mhandisi Hatari Kapufi alisema kuwa hadi kufikia Machi 2020 wakazi 1,479,750 kati ya 2,390,039 waishio vijijini walikuwa na uwezo wa kupata huduma ya maji safi kwa asilimia 62.4 kwa baadhi ya maeneo asilimia imeongezeka hadi 70.

 

Alibainisha kuwa RUWASA imeweza kutekeleza miradi mbalimbali mkoani humo kupitia programu za PbR, P4R na Mfuko wa Maji (NWF) na hadi kufikia Machi 30 mwaka huu miradi mingi inatarajiwa kukamilika.

 

Aliongeza kuwa kupitia mpango huo jumla ya miradi 31ya maji yenye thamani ya zaidi ya sh bilioni 8.7 imetekelezwa katika mkoa huo na baadhi imekamiilka na mingine iko katika hatua za mwisho.

 

Kwa upande wake Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Kaliua Mkoani hapa Salome Luhingulanya alisema kuwa serikali ya CCM inawajali sana wananchi wake hivyo akawataka wakazi wa mkoa huo kutumia vizuri miradi hiyo.