Featured Post

HALMASHAURI KALIUA YATOA MIKOPO SHILINGI MILIONI 240

MATANGAZO

Monday, December 21, 2020

SIKONGE WAKAMATA ZANA HARAMU ZA UVUVI ZENYE THAMANI YA ZAIDI YA MIL 100


 Mkuu wa wilaya ya Sikonge Mkoani Tabora Peresi Magiri (mwenye suti nyeusi) akiwa na viongozi wenzake jana wakati wa zoezi la kuteketeza zana haramu za uvuvi zilizokamatwa na Maofisa wa Idara ya Mifugo na Uvuvi wilayani humo hivi karibuni. Picha na Allan Ntana 


Na Allan Ntana, Tabora


HALMASHAURI ya wilaya ya Sikonge Mkoani Tabora imekamata zana haramu za uvuvi zenye thamani ya zaidi ya sh mil 100 na watu 7 waliokuwa wakijihusisha na vitendo hivyo wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kusababisha uharibifu mkubwa wa viumbe maji.


Akizungumza na vyombo vya habari jana Mkuu wa wilaya hiyo Peresi Magiri alipongeza halmashauri hiyo kupitia Idara ya Mifugo na Uvuvi kwa kufanya doria za mara kwa mara katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti vitendo hivyo. 


Alibainisha kuwa watuhumiwa 7 wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi watafikishwa mahakamani muda wowote kuanzia sasa ili sheria ichukue mkondo wake.


Aliongeza kuwa matumizi ya zana haramu za uvuvi ni hatari sana kwa rasilimali zilizoko katika mito na mabwawa kwa sababu hupelekea kukosekana kwa kitoweo cha samaki hivyo akatoa wito wa kukomeshwa kwa vitendo hivyo mara moja.  


Magiri aliitaka Idara ya Mifugo na Uvuvi kuendeleza doria hizo ili kuhakikisha zana haramu zote ikiwemo makokoro, nyavu, vyandarua na vinginevyo vinakamatwa na kuteketezwa ili kukomesha tabia hiyo.


Aidha aliwataka Wataalamu wa Idara hiyo kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili wajue vifaa vinavyoruhusiwa na visivyoruhusiwa kwenye uvuvi na athari za zana haramu kwa ustawi wa viumbe maji, huku akiwashauri kuhakikisha vifaa bora vya uvuvi vinapatikana kwa urahisi na kwa bei nzuri.


Awali Kaimu Mkuu wa Idara hiyo Mipawa Majebele alisema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa kutokana na doria iliyofanyika katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kudhibiti vitendo hivyo ambapo jumla ya nyavu haramu 276 na mashine 3 za kuvuta maji vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya sh mil 100 vilikamatwa.


Alisisitiza kuwa doria hiyo ni muhimu sana kwa kuwa inasaidia kuokoa viumbe maji vilivyoko katika mito na mabwawa wilayani humo kwa kuwa ni rasilimali muhimu ambayo huchochea uchumi wa wananchi kupitia uuzaji samaki.


Alibainisha kuwa doria hiyo imesaidia sana kuongeza uzalishaji wa viumbe maji hivyo kutengeneza ajira kwa wavuvi 1219 ambao wameweza kujipatia kipato cha sh mil 100 na kuiwezesha halmashauri kuingiza kipato cha zaidi ya sh mil 33.


Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Tito Luchagula alisema kuwa zoezi hilo litakuwa endelevu na wataweka utaratibu mzuri utakaosaidia wavuvi kufanya shughuli zao pasipo kubughudhiwa na mtu.


Alisisitiza kuwa hatua kali zitaendelea kuchukuliwa kwa wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo ambavyo huathiri kwa kiasi kikubwa mapato ya halmashauri ikiwemo kupunguza kitoweo cha samaki katika wilaya hiyo.

No comments:

Post a Comment