Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora Raphael Lufungija (wa tatu kutoka kulia) akiongoza madiwani wenzake wa halmashauri ya wilaya hiyo kula kiapo cha uadilifu katika kikao cha baraza hilo kilichofanyika juzi wilayani humo. Picha na Allan Kitwe.
Na Allan Kitwe, Kaliua
MADIWANI wa halmashauri ya wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora wametakiwa kuiga kasi ya utendaji wa Rais Dkt John Pombe Magufuli kwa kutekeleza wajibu wao kwa weledi mkubwa ili kuharakisha maendeleo ya wananchi wa kata zao.
Rai hiyo imetolewa juzi na Katibu Tawala wa wilaya hiyo Michael Nyahinga katika kikao cha kwanza cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo kilichoketi kwa ajili ya kumchagua Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo.
Alisema kuwa kasi na weledi wa Rais Magufuli ni kielelezo kizuri sana kwa kiongozi yeyote yule anayetaka mafanikio, hivyo akawataka madiwani hao kutekeleza wajibu wao kwa wananchi kwa vitendo na sio maneno tu.
Alisisitiza kuwa wananchi wanataka maendeleo na kutatuliwa kero zao na sio kuendekeza malumbano yasiyo na tija katika vikao vya baraza ambavyo ndivyo vyenye mamlaka ya kupitisha mipango ya maendeleo ya wananchi.
‘Nawapongeza madiwani wote mlioshinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, uchaguzi umeisha sasa kila mmoja akatekeleze wajibu wake kwa vitendo na kwa kuzingatia kanuni, taratibu na sheria’, alisema.
Katibu Msaidizi Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Magharibi, Gerald Mwaitebele aliwataka kuzingatia maadili ya utumishi na kujiepusha kumiliki mali za udharimu huku akionya kuwa yeyote atakayeenda kinyume na kiapo hicho atachukuliwa hatua za kisheria.
Naye Mwenyekiti mpya wa halmashauri hiyo Japhael Lufungija ambaye ni diwani wa kata ya Ilege (CCM) aliahidi kusimamia kwa nguvu mapato ikiwemo kuibua vyanzo vipya ili kuwezesha halmashauri hiyo kutekeleza miradi yake ya maendeleo.
Alisisitiza kuwa watashirikiana na serikali kuu kwa ukaribu zaidi ili miradi yote inayotekeleza kwa fedha za ruzuku au wahisani zitumike ipasavyo huku akionya mtumishi yeyote atakayetumia vibaya fedha hizo atakumbana na mkono wa sheria.
Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Abdallah Hemed (diwani wa kata ya Ufukutwa) alisema ili kupata maendeleo makubwa, madiwani wote wanapaswa kushikamana na kushiriki ipasavyo katika suala zima la ukusanyaji mapato.
Aidha alibainisha kuwa utekelezaji wa ahadi walizotoa kwa wananchi utategemeana sana na kasi ya ukusanyaji mapato, hivyo akatoa wito kwa madiwani na watendaji wote kufanya kazi kama timu moja.
No comments:
Post a Comment