Featured Post

HALMASHAURI KALIUA YATOA MIKOPO SHILINGI MILIONI 240

MATANGAZO

Saturday, December 26, 2020

KANISA LA KCC LAMPONGEZA RAIS MAGUFULI


 Kwaya ya Wanaume (CMF) ya kanisa la TAG Kitete Christian Center lililopo katika manispaa ya Tabora wakiimba katika ibada maalumu ya Krismas iliyofanyika katika kanisa hilo. Picha na Allan Ntana.



Na Allan Ntana, Tabora


KANISA la TAG-Kitete Christian Center lililopo katika manispaa ya Tabora limempongeza Rais Dkt.John Pombe Magufuli kwa kumtanguliza Mungu katika utawala wake na kuliwezesha taifa kuvuka salama katika kipindi kigumu cha ugonjwa wa COVID 19.


Pongezi hizo zimetolewa jana na Askofu Mstaafu ambaye pia ni Mchungaji Kiongozi wa kanisa hilo Rev. Paul Meivukie katika ibada ya sikukuu ya Krismas iliyofanyika jana kanisani hapo.


Alisema kuwa katika sikukuu hii ya kuzaliwa Yesu Kristo jamii inapaswa kumshukuru Mungu kwa mambo makubwa aliyoyafanya katika taifa letu na kwa jinsi alivyomwongoza Rais Magufuli katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu (covid-19).


Alisema kuwa mioyo ya Watanzania wote inabubujika shukrani kwa Mungu kwa jinsi Rais wetu alivyosimama katika imani na kutangaza maombi ya siku 3 ya nchi nzima kuomba dua na sala na Mungu akasikia kilio chetu na kuliponya taifa.


Kwa upande wake Mchungaji Msaidizi wa kanisa hilo Rev Shadrack Herman aliwataka Watanzania kuendelea kumtumaini Yesu Kristo na kumpa nafasi katika maisha yao ili awalee na kuwapitisha katika magumu yote wasiyoyaweza.


Baadhi ya waumini wa kanisa hilo Dkt. Zefania Zenga, Jovent William, Peter Seme na Andrew Sebastian walisema kuwa Rais Magufuli ni kiongozi na mtumishi wa Mungu, imani yake imelibeba taifa na kuokoa roho za wananchi.


Walibainisha kuwa kama sio ujasiri na imani aliyonayo kwa Mungu ugonjwa wa corona usingeisha haraka kiasi hicho na watu wengi wangepoteza maisha kama inavyotokea katika mataifa mengine.


Walibainisha kuwa Mungu ni mweza wa yote hivyo wakaitaka jamii kuendelea kumtumaini katika kila jambo ili aendelee kutenda makuu ikiwemo kudumishwa amani, upendo na mshikamano hapa nchini.


Aidha waliitaka jamii kuendelea kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa corona kwa kunawa mikono mara kwa mara huku wakisisitiza kumtanguliza Mungu katika kila jambo.


Aidha waliwataka waumini wa madhehebu yote ya dini kuendelea kumwombea Rais Magufuli na wasaidizi wake ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo na  kuharakisha maendeleo ya wananchi.

No comments:

Post a Comment