Na Allan Ntana, Tabora
HALMASHAURI ya manispaa Tabora inatarajia kuendesha msako maalumu kwa wadaiwa sugu wa mapato yatokanayo na ushuru ili kila mmoja alipe madeni yake, na watakaoshindwa kulipa watachukuliwa hatua za kisheria.
Hayo yamebainishwa juzi na Mkuu wa wilaya ya Tabora Mjini ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo Komanya Erick Kitwala alipokuwa akiongea na gazeti hili ofisini kwake.
Alisema kuwa licha ya wadaiwa hao kutakiwa kulipa madeni yao kwa wakati au kupunguza hadi watakapomaliza baadhi yao wamekuwa wakikwepa na wengine kutotoa ushirikiano jambo linalopelekea halmashauri kukosa mapato.
Alisisitiza kuwa mapato ya halmashauri ndiyo yanayofanikisha utekelezaji miradi ya maendeleo ya wananchi, hivyo hawezi kukubali watu waendelee kulimbikiza madeni tu pasipo kulipa.
Kitwala alibainisha kuwa baadhi ya watendaji wamekuwa hawatekelezi wajibu wao ipasavyo kwa kutofuatilia na kuchukua hatua stahiki kwa wale wote wanaokwepa kulipa mapato ya serikali, huku akionya kuwa Mtendaji yeyote atakayebainika kuwa chanzo cha upotevu wa mapato hayo atawajibika.
‘Tutafanza oparesheni maalumu ya kukusanya madeni kwa wadaiwa sugu wote katika maeneo mbalimbali ya manispaa, naomba kila mdaiwa sugu ajisalimishe mapema na kulipa deni lake kabla ya kuchukuliwa hatua ’, alisema.
Kwa upande wake Meya wa Manispaa hiyo Ramadhan Kapela alisema kuwa mapato mengi yamekuwa yakipotea kutokana na baadhi ya Watendaji wasio waaminifu na kutowajibika ipasavyo, hivyo akawataka kubadilika mara moja.
Alibainisha kuwa madiwani wana dhamana kubwa ya kusimamia mapato ya halmashauri hivyo akawataka kufuatilia zoezi la ukusanyaji mapato kwa Watendaji wa vijiji na kata ili watekelekeze wajibu ipasavyo.
Alibainisha kuwa miradi mingi inayotekelezwa na serikali inashindwa kukamilika kwa wakati kutokana na ufinyu wa bajeti, hivyo akawataka kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato ikiwemo kufuatilia madeni yote ili yalipwe.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Tabora mjini Emanuel Mwakasaka aliwataka madiwani hao kuwa kitu kimoja na kuhakikisha mapato ya serikali yanayokusanywa yanatumika ipasavyo.
Aidha alishauri wale wote watakaobainika kukwepa kulipa kodi hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao ili kuwezesha miradi mingi zaidi kutekelezwa ikiwemo kuwezesha vikundi vyote vya vijana, walemavu na akinamama wajasiriamali.