Featured Post

HALMASHAURI KALIUA YATOA MIKOPO SHILINGI MILIONI 240

MATANGAZO

Monday, November 30, 2020

MAKALA - NAMNA WATOTO WALIVYOKUMBUKWA WAKATI WA KAMPENI

 


Kampeni za ucharguzi mkuu mwaka huu zinaendelea kwa wagombea wa vyama mbalimbali kunadi sera zao kwa lengo la kupata nafasi za uongozi kuanzia udiwani,ubunge na Urais.

 

Katika kampeni hizo zinazotarajia kukamilika tarehe 27 mwezi huu na hatimaye wananchi kupiga kura siku inayofuata,wagombea wa vyama mbalimbali,wamekuwa wakinadi sera zao kupitia majukwaa na wananchi kuwasikiliza.

 

Hata hivyo wapo wagombea katika manispaa ya Tabora ambao wanafanya kampeni za nyumba kwa nyumba pasipo kutumia majukwaa kutokana na wao wanachokieleza kuwa kuwa ni ukosefu wa fedha.

 

Kwa wale wanaonadi sera zao kupitia majukwaa,wamekuwa wakieleza umuhimu wa michezo kwa wananchi na hasa watoto wakiwemo wanafunzi.

 

Mgombea ubunge kwa tiketi ya Chadema,jimbo la Tabora mjini,Hawa Mwaifunga,katika kampeni zake,anaeleza kuwa atatoa kipaumbele katika michezo mashuleni kwa lengo la kuibua vipaji.

 

Anaeleza kwamba chama chao katika Ilani yake,kinaeleza kuwa watashughulika na watoto shuleni kwa kuhakikisha sio tu wanapata chakula shuleni bali pia hawasomi kwenye msongamano huku wakipewa fursa ya kushiriki michezo.

 

"Tunafahamu kwamba mtoto shuleni akishiriki michezo hata ubongo wako unakuwa vizuri na hilo tutalitilia maanani"Anasema

 

Mwaifunga aliyecheza netiboli akiwa shuleni,anasema michezo hasa katika shule za msingi itapewa umuhimu na yeye kuwa mstari wa mbele kuhamasisha sanjali na kutoa misaada ya vifaa ili watoto shuleni wafurahie michezo na kupenda masomo yao.

 

Anabainisha kwamba msingi mzuri wa mtoto kimichezo ni shule za msingi na kwamba wanataka vipaji viibuliwe kuanzia ngazi hiyo ya shule za msingi na kuimarishwa sekondari.

 

Mgombea ubunge wa jimbo la Tabora Mjini kupitia CCM,Emmanuel Mwakasaka,anasema katika ilani ya CCM,michezo inasisitizwa na kupewa umuhimu mkubwa kwani ni mojawapo ya ajira.

 

Anasema katika Ilani ya Chama chake,michezo imewekewa umuhimu mkubwa kwa vile,wanataka kuibua vipaji vya watoto na kuviendeleza na kwamba ndio maana kuna michezo katika shule za msingi na sekondari ambayo wanafunzi wanashiriki.

 

Anasema pamoja na ilani yao kusisitiza kuhusu michezo,hata yeye pia ni mdau wa michezo na kwamba atakuwa mstari wa mbele kutoa vifaa vya michezo kwa watoto na wanafunzi mashuleni.

 

"Tutahakikisha watoto wanacheza kwa vile ni moja ya haki yao ya msingi katika maisha yao na tutakuwa tunawawekea msingi mzuri wa kujipatia ajira pindi wakikua kama wanavyo vipaji"Anasema

 

Naye mgombea wa jimbo hilo,kupitia CUF,Mirambo Camir,anasema chama chao kupitia Ilani kinaeleza umuhimu wa mkwa watoto na kwamba hata yeye ni mpenda michezo.

 

Anasema watoto wakiwemo wanafunzi,hawatapata shida kwa vile yeye pia ni kocha wa mpira wa miguu,akiwa amefundisha timu mbalimbali za ligi kuu na madaraja ya kwanza hadi la pili.

 

Mirambo ambaye anatumia muda mwingi kueleza sekta ya michezo majukwaani kutokana na kuwa kocha ,anasema hiyo ndio fani yake ambayo atatitumia kuibua vipaji vya watoto shuleni pamoja na kufanya majukumu yake ya ubunge.

 

Mwalimu katika shule ya Msingi ,Ipyana Daud,anasema ni muhimu watoto wakapewa kipaumbele katika kuhakikisha wanajua fursa ya kushiriki na kunufaika kupitia michezo.

 

"Ni muhimu wakafahamu namna wawakilishi wao watakavyoifanyia sekta ya michezo ambayo kwa kweli ni muhimu kwa watoto shuleni"Anasema

 

Mwanafunzi wa shule ya msingi,Samson Lucas anayesoma darasa la saba,anaeleza kwamba haelewi kama wanapaswa kufahamu namna watakavyofanyiwa na viongozi wanaochaguliwa kwa vile yeye hajihusishi na Siasa.

 

Anasema hata katika mikutano ya siasa yeye huenda kwa lengo la kuangalia wasanii kama wapo na kusikiliza wanachosema wagombea inagwa huwa hakitilii maanani.

 

"Mimi naenda kwenye mikutano kama kuna wasanii tu,sehemu ambazo hawapo huwa siendi"Anasema

 

Kwa mujibu wa Sheria ya mtoto ya mwaka 2009,watoto wana haki mbalimbali ikiwemo ya kucheza kwa kushiriki pia michezo mbalimbali na kukutana pamoja na kujifunza.

 

Sheria hiyo ni muhimu sana kwa watoto na inatoa mwongozo wa namna ya kuwatendea watoto ikiwemo kushikiriki michezo.

 

Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora,Msalika Makungu,anasema mkoa unatoa umuhimu kwa watoto kushiriki michezo na hiyo ni kutokana na mikakati na mipango ya Serikali kuona umuhimu wa michezo.

 

Anabainisha kwamba wanataka wavumbue vipaji kuanzia ngazi za chini kwa maana ya shule za msingi na ndio maana wanatoa mafunzo kwa walimu wanaowafundisha watoto wadogo mashuleni.

 

Anaeleza kwamba katika kuthamini michezo mashuleni,ndio maana kuna mashindano ya  Michezo ya shule za msingi ambapo kunakuwa na michezo mbalimbali kuanzia kwenye shule,kiwilaya,mkoa na hadi Taifa kila mwaka.

 

Afisa michezo wa Mkoa wa Tabora,Josephat Ngazime,anasema wameweka mkakati wa kuandaa kanzi data za wanamichezo katika shule za msingi lengo likiwa ni kuwatambua na kuwatumia pale wanapohitajika.

 

Anasema wanataka kufahamu ni nani ni mahiri katika mchezo gani ili iwe rahisi kuwapata na kuwatumia wanapohitajika lakini pia kuviendeleza vipaji vyao.

 

Wakazi wa Manispaa ya Tabora,wanawapongeza wagombea ambao wanaweka kipaumbele michezo kwa watoto kwa vile ndio Taifa la kesho.

 

Ibrahim Hussein mkazi wa Kanyenye,anasema kwa kuwathamini watoto,wagombea wanaweka katika mazingira chanya kwani wanapomaliza masomo yao,watakuwa katika nafasi nzuri ya kutuia vipaji vyao wanapokuwa.

 

Naye Maimuna Seleman mkazi wa Isevya,anashukuru baadhi ya wagombea kuona umuhimu wa kukuza sekta ya michezo kwa vile ni ajira nzuri na inayolipa vizuri.

 

"Sasa hivi ajira serikalini ni tatizo kubwa hivyo tunaona sehemu ya kuwafanya watoto wetu wafanikiwe kimaisha ni kupitia sekta ya michezo"Anasema

 

Kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka huu,zinatarajia kumalizika tarehe 27 na uchaguzi kufanyika tarehe 28 mwezi huu huku ajenda mbalimbali zikielezwa na vyama vya Siasa kwa lengo la kuwashawishi wapiga kura wawachague.

 

No comments:

Post a Comment