Robert Kakwesi,Tabora
Makala-Manufaa waliyopata watoto wakati wa likizo ya Corona
Tanzania kama nchi nyingine duniani ilipata wagonjwa wa Homa kali ya mapafu maarufu kama corona,ugonjwa uliochukua maisha ya mamilioni ya watu katika nchi mbalimbali Tanzania ikiwemo.
Sanjali na kuua watu,ugonjwa huo pia uliwafanya maelfu watu dunia kuugua na kufanya watu kubadili mfumo wa maisha kwa lengo la kuukwepa ugonjwa huo ambao ulielezwa hautaki msongamano wa watu.
Kutokana na athari zake,Tanzania iliachukua uamuzi wa kuzifunga shule zake zote kuanzia za awali hadi Vyuo Vikuu na wanafunzi kutakiwa kwenda likizo mwezi wa tatu hadi mwezi wa sita mwaka huu.
Wakati wa likizo,Serikali ilitoa maagizo kadhaa kwa watoto ikiwemo kukaa majumbani na kuwataka wazazi na walezi kuwaangalia kwa karibu watoto wao ili wasipate maambukizi ya ugonjwa huo hatari.
Kuna msemo usemao kuwa katika jambo baya pia kuna uzuri wake na ndio maana pamoja na ugonjwa huo kuchukua maisha ya watu na kuhatarisha uchumi wa nchi nyingi duniani kulikuwa na mazuri yake kwa watoto.
Dkatari wa watoto katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora,Kitete,Dr Mnubi Baguma,anasema mtoto anapopa muda mwingi wa kuwa na mzazi wake anapata furaha na amani na hivyo kukua vizuri.
Anasema malezi mazuri anayopata kutoka kwa wazazi wake yanamjenga kiakili na kuwa na ubongo unaochemka tofauti na mtoto asiyepata malezi mazuri na kula vizuri kutoka kwa mzazi wake.
Anabainisha kuwa mtoto anapokuwa mbali na wazazi wake,kisaikolojia huathirika kwani anakuwa najenga imani kubwa kwa wazazi wake na anaposononeka,anapata wakati mgumu na akili yake kuathirika kwa namna moja au nyingine na hivyo kuweza kuathirika pia kimasomo.
“Mtoto anayeishi vizuri na wazazi wake na kupata malezi bora,hata ukuaji wake na akili yake unakuwa tofauti na wengine wasiopata anayopata”Anasema.
Askofu wa Anglican Dayosisi ya Tabora,Elias Chakupewa,anasema katika kipindi cha likizo ya ugonjwa huo,wazazi na walezi walipata muda zaidi wa kuwasoma tabia watoto wao tofauti na kabla ya ugonjwa huo.
Anasema ni muhimu wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wao kwa lengo la kuwafundisha tabia njema na kuwasoma mienendo yao.
Mzazi Lucas Simon,anakiri likizo ya ugonjwa huo kumfanya kuwa karibu zaidi na watoto wake na hivyo kuwafahamu tabia zao zingine ambazo alikuwa hazifahamu.
“Tulikuwa na wakati mzuri baada ya kuondolewa wasiwasi kuhusu ugonjwa huo na kwangu tulikaa vizuri sana na kufurahi na watoto wangu wa darasa la tano na la tatu”anasema
Mwanafunzi Hadija Baraka wa shule ya msingi Kitete,Manispaa ya Tabora anayesoma darasa la sita,anasema wazazi wake walichukua jukumu la kuwafundisha nyumbani tofauti na zamani.
Anaeleza kwamba hakuwahi kufundishwa na wazazi wake kwani anaporudi nyumbani hakuwa akiwakuta na wanaporudi inakuwa wakati wa usiku wao wakiwa wamelala.
“Wazazi wangu ni watumishi wanaosafiri sana lakini wakati wa likizo ya corona tulikuwa tunashinda nao nyumbani”Anasema
Mwanasheria Charles Ayo,anasema mtoto ana haki ya kucheza na kufurahi na kipindi cha likizo ya corona,watoto wengi walipata muda zaidi wa kucheza na kufurahi.
Kwa mujibu wa sheria ya mtoto ya mwaka 2009,mtoto ana haki ya kucheza na hilo wazazi walilitekeleza vizuri ingawa hawakupata muda mzuri wa kushiriki kikamilifu na wenzao.
Anabainisha kuwa kwa mtoto kucheza na kufurahi anapata amani ya moyo na hata akili na ukuaji wake unakuwa ni mzuri tofauti na wale wasiocheza au kushiriki furaha utotoni.
Mtaalamu wa saikolojia ya watoto,aliyeomba hifadhi ya jina lake,anasema malezi huchangia kwa kiasi kikubwa akili na ukuaji wa mtoto.
Anaeleza kuwa malezi anayopata mtoto ni kuanzia chakula anachokula,namna anavyolelewa katika maisha yake kuwa yanachangia kuwa na akili nzuri na mwili mzuri.
“We angalia watoto wasiolelewa vizuri wengi wanakuwa na utapiamlo na akili inakuwa ni changamoto”Anasema.
Anasisistiza kuwa wakati wa likizo ya corona,wazazi na walezi wale waliokaa vizuri na watoto wao,watakuwa walichangia kuongezeka akili na ukuaji wao kikamilifu,akisistiza mtoto anafurahi kuwa karibu na mzazi wake.
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora,Aggrey Mwanri,aliagiza watoto kufundishwa kupitia njia ye redio zilizopo Manispaa ya Tabora na watoto kujifunza.
Anasema pamoja na changamoto zake lakini ilisaidia kwa baadhi ya watoto kujifunza kwa njia hiyo jambo lilikuwa geni kwao kwa mara ya kwanza.
Mwanafunzi Iddy Hassan wa shule ya msingi Kanyenye,anasema hakuwa na utaratibu wa kusikilia redio lakini wakati wa likizo ya corona ndio aliweka katika ratiba yake kuwa anasikiliza redio.
“Hadi leo hii mimi ni mpenzi wa kusikiliza redio baada ya kujenga utamaduni wa kusikiliza redio katika vipindi vilivyokuwa vinafundishwa na kupata fursa ya kusikiliza vipindi vingine pia”Anasema
Aliyekuwa afisa elimu wa Mkoa wa Tabora,Suzan Nusu,anasema ufundishwaji wa vipindi kupitia redio ulikuwa haujazoeleka kwa wanafunzi wengi na ilikuwa changamoto kubwa kwao ambayo walijaribu kuitumia kwa manufaa yao.
Anasema kama ungeendelea kwa kipindi kirefu ilikuwa lazima mambo yaendelee na ndio maana waliamua kuwa na njia mbadala kujiandaa kikamilifu hata kama ungechukua muda mrefu.
Afisa elimu Manispaa ya Tabora,Joel Mkuchika,anasema wakati wa likizo ya corona,walikuwa wakiwasiliana na watoto na wazazi kikamilifu kwa lengo la kuwasaidia katika masomo na kujikinga na ugonjwa huo.
Anasema mawasiliano yalikuwa ya karibu zaidi tofauti na zamani na wazazi na walezi wengi walikuwa wakitaka kufahamu namna watoto wao watakavyoendelea kujifunza wakiwa nyumbani.
Kikubwa kwake ni kuona namna wazazi na walezi walivyouona ukweli wa kazi kubwa na nzuri inayofanywa na walimu katika kuwalea watoto wao wawapo shuleni.
Anasema wengi waliona ugumu wa kuwa na watoto wao nyumbani muda mwingi na kutupa pongezi kuwa tunafanya kazi nzuri sana nay a manufaa kwao na Taifa kwa ujumla.
Anabainisha kuwa somo walilojifunza wazazi na walezi kuhusu ugumu wa kuwatunza watoto ni furaha kwao kwani wana uhakika sasa watapata ushirikiano mkubwa zaidi kutoka kwao tofauti na zamani.
Serikali ya mkoa iliweka mkakati maalum kuhakikisha watoto hawapati maambukizi wakiwa nyumbani na hivyo kuweka mikakati mbalimbali ikiwemo kukataza watoto kutembea ovyo pamoja na wazazi na walezi kutakiwa kufuata masharti yote ya kujikinga na ugonjwa huo.
Nyumba zote zililazimishwa kuwekwa ndoo ya maji ya kunawa milangoni ili itumiwe na wote wanaopita pamoja na wale wanaoishi ndani ya nyumba husika.
Afisa ustawi wa Jamii Manispaa ya Tabora,Rehema Maembe,anasema wazazi na walezi wengi walikuwa hawatimizi wajibu wao kikamilifu na likizo hiyo, imewakumbusha kutimiza kikamilifu wajibu kwa watoto wao.
Kutokana na baadhi ya manufaa ambayo wazazi na watoto wameyapata wakati wa likizo ya ugonjwa wa corona,ni imani kubwa kuwa kutakuwa na mabadiliko ya mahusiano kati ya wazazi/walezi kwa upande mmoja na walimu na pia watoto na wazazi/walezi wao kwa upande mwingine na hivyo kila mmoja kutimiza wajibu wake kwa manufaa yake na jamii kwa ujumla.
Kwa watoto kupata uzoefu tofauti na kulelewa na wazazi na walezi wao kwa muda mrefu,wanakuwa wamefurahi na kwa kujifunza kwa njia tofauti,kuimarisha ubongo na kupata akili zaidi huku wakiwa na uhakika wa kukua katika namna inayowaweka vizuri kimwili kutokana na malezi waliyopata na wanayoendelea kuyapata kutoka kwa wakubwa zao kiumri.
No comments:
Post a Comment