Mwenyekiti wa chama cha Soka Manispaa ya Tabora Samwel Malle akiwashukuru wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi kwa kumchagua yeye na viongozi wengine.Picha na Allan Ntana.
Na Allan Ntana, Tabora
CHAMA cha soka wilayani Tabora, Mkoani hapa (TUFA) kimepata viongozi wapya watakaokiongoza kwa kipindi kingine cha miaka minne baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu na wajumbe wa Kamati tendaji.
Akiongea na gazeti hili baada ya kukamilika kwa uchaguzi huo na matokeo kutangazwa, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi Pankras Kaikai Bwena alimtangaza Mwandishi wa habari za michezo wa kituo cha redio VOT FM Samwel Malle kuwa mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti kwa kupata kura 28 dhidi ya kura 21 alizopata mpinzani wake Amani Seifu.
Aidha Andrew Zoma aliibuka kidedea katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti baada ya mgombea pekee aliyekuwepo kujitoa kwenye kinyang’anyiro hicho kwa madai ya kubanwa na majukumu mengine.
Bwena alimtangaza Mwalimu Awadh Sabuni Said kuwa Katibu wa chama hicho baada ya kupata kura za ndio 40 na nafasi ya Katibu Msaidizi akatangazwa Paschal Herman aliyekuwa mgombea pekee kwa kupata kura zote 40.
Aidha alimtangaza Abdallah Mgemwa kuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa chama cha soka mkoa wa Tabora (TAREF) kwa kupata kura 31 dhidi ya 18 alizopata mpinzani wake Geofrey Mabele.
Kwa upande wa soka la wanawake, msimamizi alimtangaza Frola Kadamanja kuwa Mwakilishi wa TAREFA baada ya kupata kura za ndio 48, huku Henry Richard Kitundu akichaguliwa kuwa mwakilishi wa vilabu kwa kupata kura za ndio 48.
Bwena alibainisha kuwa kwa nafasi ya ujumbe wa Kamati tendaji ya chama hicho ilichukuliwa na Willson Msonzela aliyepata kura 45 na Martin Enock aliyepata kura 48.
No comments:
Post a Comment