Na Robert Kakwesi
MCHAKATO wa kuwapata viongozi wa ngazi mbalimbali kwenye uchaguzi Mkuu mwaka huu unafikia mwisho tarehe 28 mwezi huu pale watakapopatikana viongozi watakaochaguliwa na wananchi.
Viongozi hao kuanzia madiwani,wabunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,watapatikana baada ya kufanyika kampeni iliyochukua miezi miwili kwa wagombea kunadi sera za vyama vyo kwa lengo la kuwashawishi wananchi wawachague.
Katika wagombea wanaonadi sera za vyama vyao,wanaeleza kuwa Ilani za Vyama vyao kimsingi zinaeleza mambo muhimu atakayofanyiwa mtoto kuanzia mama yake anapokuwa mjamzito hadi anapozaliwa na kukua.
Mgombea waChama Cha Mapinduzi (CCM) jimbo la Tabora Mjini,Emmanuel Mwakasaka,anasema Ilani ya Chama chake inaeleza mtoto kupewa stahiki zake kwa kuangaliwa mzazi wake ambaye anapatiwa huduma tangu awapo tumboni.
Anasema kuwa mzazi anapatiwa chanzo kwa mujibu wa sera ya Afya ambayo inahimiza kila mjamzito kupata chanjo mbalimbali za kumkinga mtoto na magonjwa.
Anabainisha kwamba akinamama wajawazito kwa mujibu wa mwongozo wa Afya katika sehemu za kutolea huduma kuwa hawatakiwi kutozwa chochote kwani huduma za kujifungua ni bure.
Hata hivyo, anasema kuna athari za kupata mtoto kimakuzi kama hataandaliwa msingi mzuri katika makuzi yake na hilo chama chake imeliona na ndio maana kuna sera na miongozo mbalimbali ya kushughulika na watoto.
“Hili la watoto chini miaka mitano kuhudumiwa bure na wazee ni maalum kuhakikisha watoto wanapata makuzi mazuri ili wawe raia wema baadaye wenye afya njema,” anasema.
Mgombea udiwani wa kata ya Kanyenye,Manispaa ya Tabora,Donatus Rupoli,anasema chama chake cha Chadema, kinatoa msisitizo kwa watoto kupata huduma bora katika makuzi yao kuanzia nyumbani hadi awapo shuleni.
Anasema hawataki mtoto akue katika mazingira mabaya kwa vile wanajua athari zake kuwa anaweza kudhurika kiafya na kushindwa kutoa mchango wake kwa Taifa ipasavyo.
Anasema akiwa diwani atahakikisha watoto wanapata huduma bora tangu wanapozaliwa na hata kabla ya kuzaliwa ili wakue katika makuzi mema na kuwa na afya nzuri.
Mkazi wa kata ya Ng’ambo,Zubery Abdallah,anasema bahati mbaya sana wagombea wengi katika nafasi za udiwani,ubunge na hata urais hawaelezi kuhusu namna watakavyoshughulika na mtoto kimakuzi.
“Tunataka watueleze ni kwa namna gani watatuhakikishia watoto wetu wanapata makuzi bora na sio tu kusema matibabu bure,” anasema
Naye Lucas Yohana mkazi wa Chemchem,anabainisha kwamba kwa sasa watoto wanapata chanjo kwa uhakika jambo wanalolifurahia, ingawa dawa kwa watoto wadogo chini ya umri wa miaka mitano ni tatizo.
Anaeleza kwamba serikali imeweka mwongozo mzuri wa watoto wa umri huo kupata matibabu bure, lakini kiuhalisia hilo halifanyiki katika sehemu za kutolea huduma za afya,” anasema.
“Ukienda vituo vya kutolea huduma unaambiwa hakuna dawa labda panadol tu sasa hili halijaa vizuri,” anasema.
Anasema kama matibabu ni bure basi na madawa yawe yanapatikana vinginevyo ni kiini macho, kwani kama mzazi hana fedha,afya ya mtoto inakuwa mashakani.
Kwa ufupi wazazi wanataka wahakikishiwe uhakika wa watoto kupata ulinzi kimatibabu kuanzia pale mimba inapotungwa hadi angalau anapofikisha umri wa miaka mitano
Daktari wa watoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora,Kitete,Dk. Mnubi Baguma,anasema kuna athari kubwa kwa watoto ambao hawalelewi katika mazingira mazuri na salama.
Anasema mtoto mbali ya kutakiwa kulelewa katika mazingira mazuri,anapaswa kupata maziwa ya kutosha kutoka kwa mama yake na kama mama atakuwa na msongo wa mawazo,kamwe hawezi kutoa maziwa ya kutosha.
“Maziwa ya mama pia hutegemea saikolojia yake achilia mbali chakula anachokula,” anasema.
Anaeleza kuwa kuna athari kwa mtoto anayelelewa katika mazingira yasiyo salama kwa vile athari zake kimakuzi ni mbaya kwani anaweza kuwa mzito darasani kujifunza ukilinganisha na yule anayelelewa katika mazingira mazuri. “Maziwa ya mama kwa kipindi cha miezi sita yanatengenezwa kwa namna yake kiasi kwamba mahitaji yote ya mtoto yapo yakiwemo maji,” anasema.
Dk. Baguma anaeleza kwamba baada ya miezi sita ndiyo mtoto anaweza kuanza kupewa vyakula vingine huku akiendelea kunyonya hadi anafikisha miaka miwili au mitatu kutegemea hali yake.
Anaeleza kwamba mtoto huanza kujengwa tangu mimba inapoingia, ambayo ni msingi mkuu wa maisha yake,yanayoendelea pale mimba inapokua kisha kuzaliwa hadi anafikisha miaka mitatu hadi mitano.
“Msingi mkubwa wa mtoto kimakuzi na kiakili huanza kujengwa mimba inapotungwa,kulelewa hadi kuzaliwa na kuendelea wakati akinyonya mpaka anapoacha kunyonya,” anasema.
Ni dhahiri kuwa msingi wa makuzi ya akili ya mtoto anayeishi katika mazingira magumu unakuwa haupo vizuri,ambapo hupata msingi mbaya wa maisha yake.
Anasisistiza kuwa akili ya mtoto humuathiri hata akikua na kuanza shule kwani anakua hajiamini na kujitenga sababu anakuwa anajengwa na kuathirika akiwa tumboni au baada ya kuzaliwa,akiongeza kuwa mara nyingi huathirika hadi utu uzima wake.
Kutokana na athari za mtoto kitaalamu kwa mujibu wa Dk. Bagumani vizuri kwa wagombea siyo tu kuweka msingi mzuri kwa makuzi ya mtoto bali hata mazingira ya wazazi watarajiwa na wazazi wenye watoto.
Mtaalamu wa elimu ya malezi kwa makuzi ya mtoto,Ofisa Muuguzi katika zahanati ya Mjini Tabora,Catherine Mushi,anasema elimu hiyo ni muhimu kwa vile inamsaidia kukua kimwili,kiakili,kihisia na kijamii. Anaeleza kuwa elimu hiyo huanzia tangu ujauzito hadi umri wa miaka mitatu.
Mushi anabainisha kuwa mtoto anajifunza kutambua rangi na vitu mbalimbali,akisisitiza elimu ya utambuzi huanzia nyumbani na siyo sehemu nyingine yoyote,jambo linalodhihirisha watoto walio mahabusu au gerezani hukosa fursa hiyo muhimu.
Anabainisha kuwa pamoja na wazazi kutakiwa kuzungumza na watoto wao wangali tumboni na baada ya kuzaliwa,bado wanahitajika kucheza nao michezo mbalimbali na kuwaimbia.
Ni wazi kuwa kwa mama mwenye msongo wa mawazo anayeugua ugonjwa wa sonona,kutokana na madhila aliyopata,hawezi kufanya hayo kwa mtoto kutokana na hali yake na mazingira na hivyo kumkosesha msingi mzuri wa makuzi yake.
Mushi anabainisha kuwa tafiti za watoto zinaonesha wale waliopewa msingi bora wa malezi kuanzia utungwaji mimba,inapolelewa hadi anapotimiza miaka mitatu,huwa na tabia nzuri na hazibadiliki hata wakiwa wakubwa.
Mwanasheria wa asasi isiyo ya Kiserikali ya Jamii Salama Development Volunteer,JSDVambayo inajishughulisha na utoaji elimu ya sheria kwa wasaidizi wa kisheria,Paralegal,Charles Ayo,anasema sheria ya mtoto ya mwaka 2009 inakataza mtoto kutwezwa au kushushwa utu wake. Wagombea wanapaswa kuhakikisha wanalinda haki za mtoto.
Anasisitiza kwamba watoto ni Taifa la baadaye na kama wakiwekewa msingi mzuri,watakuwa na manufaa kwa Taifa na kutaka wagombea na vyama vyao kutoa umuhimu katika makuzi na malezi ya mtoto.
Mkataba wa kimataifa wa watoto (CRC) wa mwaka 1989,unataka watoto kuanzia ujauzito hadi wafikishapo miaka mitatu kupata lishe bora, ulinzi na mahitaji bora kwa ajili ya makuzi yao na kuimarisha ubongo.
Ni dhahiri kwamba kwa watoto wanapaswa kupewa haki haki zao kikamlifu ikiwamo kupata lishe bora katika maisha yao.
Hivyo kutokana umuhimu wa mtoto ambaye ni Taifa la baadaye,kupata stahiki na haki yake ya kuishi katika makuzi bora na kulelewa vema na wazazi au walezi wao, wagombea pamoja na vyama vyao vya Siasa,wanapaswa kutambua kuwa jambo hilo ni muhimu na linalopaswa kuwekwa msisitizo katika Ilani za Vyama vyao,sera na mipango yao kama wagombea.