WAKULIMA wa zao la tangawizi wa kijiji cha Mnzeze kata ya Mnzeze, tarafa ya Manyovu wilayani Buhigwe Mkoani Kigoma wameomba serikali kuwasaidia kutafuta wawekezaji ili kuwajengea kiwanda cha kuchakata zao hilo.
Ombi hilo limetolewa jana na wakulima wa zao hilo kutoka wilayani humo walioshiriki katika maonesho ya wakulima nane nane Kanda ya Magharibi yaliyomalizika jana katika uwanja wa Fatma Mwassa mjini Tabora.
Walisema kuwa zao hilo linalimwa kwa wingi sana katika kata hiyo yenye vijiji 4 vya Mnzeze, Kishanga, Kigogwe na Mrungu ambapo zaidi ya asilimia 90 ya wakazi wote wa kata hiyo wanalima zao hilo.
Ezekiel Joseph (46) mkulima mkazi wa kijiji hicho alisema kuwa kilimo cha zao hilo kimewanufaisha sana wananchi kwa kuwa hakina gharama kubwa na ni zao linalostahimili ukame kwa kiasi kikubwa.
Alitoa mfano wa msimu wa mwaka jana ambapo alilima ekari 2 na kufanikiwa kuvuna ya tani 16 za zao hilo ambazo zilimwezesha kupata kiasi cha sh mil 9 na kwa mwaka huu amelima jumla ya ekari 4 ambapo anatarajia kuvuna tani 32.
‘Tangawizi inastawi sana hapa Buhigwe, lakini changamoto yetu kubwa ni masoko na ukosefu wa viwanda vya kuchakata zao hilo, tunaomba serikali itusaidie kupata wawekezaji waje kutujengea kiwanda ili kuongeza thamani yake’, alisema.
Naye Amos Kayage mkulima kutoka kijiji cha Kishanga alisema kuwa zao hilo ni la biashara, hivyo kama watapata soko zuri au kiwanda watainuka sana kiuchumi na kuchangia kwa kiasi kikubwa mapato ya halmashauri yao.
Alibainisha kuwa zao la tangawizi likichakatwa kwenye mashine linaweza kutoa mazao mengi ikiwemo unga, mbolea na mengineyo tofauti na hali ilivyo sasa, hivyo akaomba wataalamu wawape elimu zaidi ili kuboresha kilimo hicho.
Ofisa Kilimo wa halmashauri hiyo Mjairi Baraka alikiri kuwa zao hilo limewapa manufaa makubwa wakazi wa vijiji vya kata hiyo na kata jirani za Janda na Kinazi ambapo kwa wastani wanavuna hadi tani 1200 kwa mwaka ila changamoto yao kubwa ni masoko, ila juhudi za kutafuta masoko zinaendelea.
Aliongeza kuwa licha ya uhaba wa masoko kile kidogo wanachouza katika maeneo mbalimbali ikiwemo nchi jirani za Burundi, Rwanda na Kongo kimewasaidia sana kwani wengi wao wamejenga nyumba nzuri, kununua pikipiki na hata magari.
No comments:
Post a Comment