Featured Post

HALMASHAURI KALIUA YATOA MIKOPO SHILINGI MILIONI 240

MATANGAZO

Thursday, August 13, 2020

UTAFITI TAASISI ZA KILIMO KANDA YA MAGHARIBI WAMKUNA RC ANDENGENYE

 Na Allan Ntana, Tabora


MKUU wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Msaidizi Thobias Andengenye amefurahishwa na utafiti wa mbegu za mazao unaofanywa  na taasisi za kilimo zilizoko Mikoa ya Tabora na Kigoma.


Akizungumza katika kilele cha maonesho ya wakulima nane nane Kanda ya Magharibi yaliyomalizika jana katika uwanja wa Fatma Mwassa uliopo eneo la Ipuli mjini Tabora alisema kuwa utafiti na elimu iliyotolewa na taasisi hizo imeleta tija kubwa kwa wakulima.


Alibainisha kuwa kuanzishwa kwa vituo vya utafiti wa mazao kumekuwa msaada mkubwa sana kwa wakulima kutokana na ushauri mzuri wa kitaalamu, ubunifu na dhamira njema ya kuwainua wakulima.


Andengenye alitaja taasisi ambazo zimeleta mageuzi makubwa ya sekta ya kilimo na kuanza kunufaisha wakulima kuwa ni pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Taasisi ya Utafiti wa zao la Kahawa (TACRI) na kampuni ya Felisa.


‘Tumejipanga vizuri ili kuhakikisha kilimo cha mazao ya kimkakati kinaendelea kupewa kipaumbele kikubwa katika wilaya zote za mikoa hiyo ikiwemo kuboreshwa kwa teknolojia na kusisitiza matumizi ya mbegu bora’, alisema.


Alitoa wito kwa wadau na taasisi mbalimbali hapa nchini kuja kuwekeza katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi katika Kanda hiyo ikiwemo kutoa elimu ya kilimo kwa wakulima.


Aidha alisisitiza kuendelea kuimarishwa kwa bodi za mazao na kuboreshwa kwa miradi ya ufugaji samaki katika halmashauri zote za mikoa hiyo huku akiwataka wananchi kutumia ipasavyo ujuzi na elimu waliyopata katika maonesho hayo.


Awali Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt Philemon Sengati alisema kuwa ndoto yake ni kuona maonesho ya wakulima nane nane katika Kanda hiyo yanakuwa ya mfano wa kuigwa na kanda zingine na ikiwezekana mwakani maonesho ya kitaifa yafanyikie hapo.


Aliongeza kuwa dhamira yake ni kuona maonesho ya ukanda huo yanakuwa mashamba darasa na bidhaa zote zinazoletwa ziwe na tija kubwa kwa wakulima, jamii, nchi na mataifa mengine kwa ujumla.


No comments:

Post a Comment