Featured Post

HALMASHAURI KALIUA YATOA MIKOPO SHILINGI MILIONI 240

MATANGAZO

Tuesday, June 16, 2020

WAGANGA TIBA ASILIA WATAKIWA KUWA WABUNIFU

Wazee  wa  Kimila  na  Waganga  wa Tiba  mbadala  wilayani Kaliua mkoani Tabora


Na Allan Ntana, Tabora

WAGANGA wa tiba asilia wilayani Kaliua Mkoani Tabora wameshauriwa kuongeza ubunifu katika utoaji huduma za tiba mbadala ili kuisaidia serikali katika kukabiliana na magonjwa hatarishi ya mlipuko ikiwemo ugonjwa wa corona.

Ushauri huo umetolewa jana na Ofisa Tarafa wa tarafa ya Kaliua Bethord Mahenge alipokuwa akifungua mkutano wa Chama cha Wazee wa Kimila wilayani humo kwa niaba ya Mkuu wa wilaya hiyo Abel Busalama.

Aliwataka Wazee wa Kimila kwa kushirikiana na Waganga wa tiba asilia kuendelea kubuni tiba mbadala zitakazosaidia kukabiliana na magonjwa yasiyo na dawa kama vile ukimwi na homa kali ya mapafu (covid 19).

Alisisitiza kuwa dawa za asili ni tiba mbadala yenye uwezo mkubwa wa kutibu magonjwa mbalimbali miongoni mwa jamii, tatizo lililopo ni kukosa ubunifu kwa wahusika na wengine kuingiza ujanja ujanja usiokuwa na tija kwa jamii.

Mahenge alibainisha kuwa baadhi ya waganga wamekuwa sio waadilifu katika kazi zao na wengine wamekuwa sio wa kweli jambo linalopelekea kutoaminika kwa huduma wanazotoa miongoni mwa jamii.

‘Ndugu zangu tuache tamaa ya fedha katika kutekeleza wajibu wetu, tusaidie jamii kwa moyo wa dhati, toeni taarifa za wale wanaoendekeza ulaghai na kuwaibia wananchi ili wasiendelee kuchafua chama chenu’, alisema.

Mahenge alitoa wito kwa waganga wa tiba asilia na wazee wa kimila kumtanguliza Mwenyezi Mungu katika kazi zao na kuwa marafiki wa serikali kwa kufichua wahalifu na kukomesha vitendo hivyo miongoni mwa jamii.

Ili kukomesha tabia za ulaghai miongoni mwao aliwataka kuhakikisha kila mmoja anajiandikisha ili ijulikane anakoishi na uongozi wa chama hicho umtambue ili atakapopata matatizo aweze kupata msaada.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Mwanahamisi Juma alipongeza Chama cha Wazee wa Kimila wilayani humo kwa mwamko wao wenye dhamira ya kukomesha na vitendo vya unyanyapaa kwa watoto na akinamama.

 Ili kufanikisha majukumu yao ya kila siku aliwataka kufuata sheria, kanuni na taratibu na kujiepusha na ramli chonganishi kwa kuwa zinaongeza uhasama na chuki miongoni mwa jamii.

No comments:

Post a Comment