Featured Post

HALMASHAURI KALIUA YATOA MIKOPO SHILINGI MILIONI 240

MATANGAZO

Tuesday, June 16, 2020

DED KALIUA ATOA MOTISHA KWA WALIMU SHULE YA MSINGI UGANSA



Na Allan Ntana, Tabora                                                                        
MKURUGENZI Mtendaji wa halmshauri ya wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora Dkt John Marco Pima ametoa motisha ya fedha taslimu zaidi ya sh 160,000 kwa walimu wa shule ya msingi Ugansa iliyoko katika kata ya Usinge kwa kufaulisha wanafunzi wote.

Akizungumza na mwandishi wetu, Dkt Pima alisema kuwa motisha hiyo imetolewa hivi karibuni kama pongezi kwa walimu wa shule hiyo baada ya kuiwezesha kuwa ya kwanza kiwilaya kwa miaka 2 mfululizo katika matokeo ya darasa la saba.

Aliongeza kuwa juhudi kubwa zilizooneshwa na walimu hao wakiongozwa na Mwalimu Mkuu Cosmas Seleka Leonard zimewezesha watoto wote waliomaliza darasa la saba 2018 na 2019 kuchaguliwa kujiunga na shule za sekondari.

Dkt Pima alieleza kuwa utendaji wa walimu wa shule hiyo ni mfano wa kuigwa na shule nyingine na kuahidi kuendelea kuwapa motisha, kwani licha ya kuwa kijijini imeshika nafasi ya 6 kimkoa na kushindana na shule za mchepuo wa kingereza.

‘Nimetoa motisha ya sh 100,000 kwa ajili ya shule, nimetoa zaidi ya sh 50,000 kwa idadi ya alama ‘A’ za kila somo ambazo mwalimu wa somo husika alipata na sh 50,000 kama motisha kwa uongozi wa shule’, alisema.

Naye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Cosmas Seleka alifafanua kuwa mwaka 2018 wahitimu wa darasa la 7 katika shule hiyo walikuwa 78 na mwaka 2019 walikuwa 70 na wote walifaulu mitihani yao ya mwisho na kujiunga na shule za sekondari.

Aidha alimshukuru Mkurugenzi kwa kutoa zawadi kwa walimu wote waliofaulisha kwa kiwango cha ‘A’ katika somo lolote ambapo kila A alitoa sh 500/- , walimu zaidi ya 15 walijipatia kifuta jasho cha fedha taslimu kulingana na idadi ya A zilizopatikana kwenye somo lake.

Akilezea siri ya mafanikio hayo, Mwalimu wa Taaluma shuleni hapo Mwalimu Malundi Stefano Malundi alisema kuwa ushirikiano wa dhati baina ya walimu na usimamizi madhubuti wa ratiba ya vipindi vya darasani ndio siri ya matokeo hayo.

Aliongeza kuwa walimu wote wanajali sana muda kwani wanaamka saa 11 alfajiri na kujiandaa na kila siku vipindi vinaanza saa 1.00 asubuhi na watoto wanakaa shuleni hadi saa12.00 jioni wakiwa na walimu wao.

No comments:

Post a Comment