Featured Post

HALMASHAURI KALIUA YATOA MIKOPO SHILINGI MILIONI 240

MATANGAZO

Wednesday, June 24, 2020

TUMBAKU ILIYOKUWA ICHOMWE MOTO KUWAFUTA JASHO WAKULIMA

Wafanyakazi Mjini Urambo,wakipakia magunia ya tumbaku ambayo ilikuwa ichomwe moto na bodi ya tumbaku ambayo kwa akutochomwa moto sasa itawaingizia wakulima zaidi ya Sh2.3bilioni.
picha na Robert Conrad.


Robert Conrad,Tabora.
Tabora.Bodi ya tumbaku nchini,TTB,imefanikisha kununuliwa tumbaku iliyozidi makisio ambayo ilipaswa kuchomwa moto kutokana na kutokuwa katika hali nzuri huku ikiwa na wadudu na hivyo kufanya wakulima kupata zaidi ya Sh2.3bilioni ambazo wasingezipata kama tumbaku hiyo ingechomwa moto.
Akizungumzia kuhusu suala hilo,kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Tumbaku nchini,TTB,Stan Mnozya,alisema,Tumbaku hiyo inanunuliwa na Kampuni ya Alliance One baada ya mazungumzo na bodi ya Tumbaku,ambapo kiasi cha zaidi ya kilo milioni moja na nusu zenye thamani ya Sh2.3bilioni zitalipwa ,pesa ambazo  kama Bodi ingetumia sheria wakulima wasingezipata.
"Kutokana na hali ya tumbaku ilivyokuwa na kwa kufuata sheria na kanuni zetu ilikuwa tumbaku hiyo tuichome moto lakini wakulima watu wangepoteza kiasi hicho cha pesa"Alisema
Mnozya aliongeza kuwa tumbaku hiyo ilikuwa ni miongoni mwa kilo 12.8milioni zilizozidi makisio msimu uliopita lakini waliweza kuzishawishi kampuni za ununuzi wa tumbaku kuzinunua ingawa kwa bei ya chini na kubaki kiasi cha kilo milioni 1.8 ambazo ndio hizo zilianza kuharibika na zingine kuingiliwa na wadudu.
Alisema kampuni hiyo itawekea dawa tumbaku hiyo na kwamba wanainunua kwa bei ya US Dola 0.58 wastani kwa kilo ambazo angalau wakulima watapata kuliko kukosa kabisa.
kuhusu wakulima ambao tumbkau iliyozidi makisio ilinunuliwa na kampuni moja kutoka nje ambayo haikuwalipa kutokana na tatizo la ugonjwa wa corona,alisema kuwa nao kama kampuni hiyo haitawalipa watalipwa.
Alieleza kuwa kampuni hiyo,viongozi wake walizuiliwa nje ya nchi kutokana na zuio la ugonjwa wa corona na hivyo kushindwa kumalizia mchakato wa kuwalipa wakulima baada ya kununua tumbaku yao iliyozidi makisio.
"Tutatumia mwanya huu kuhakikisha wakulima ambao tumbaku yao ilikuwa inunuliwe na kampuni hiyo,wanalipwa kwani hii iliyobaki inanunuliwa yote"Alisema
Wakulima walisema wanaishukuru bodi ya tumbaku kwa kuwahangaikia na angalau kupata kiasi hicho cha pesa kwani hawakuwa na matumaini kabisa ya kupata angalau kidogo.
"Nitatumia pesa nitakazolipwa kwa kuweka maisha yangu vizuri hasa kipindi hiki cha ugonjwa wa corona unaosumbua duniani na nchini kwetu"Alisema Erasto Mahona mkulima wa Urambo
Naye Jaffary Kankila,alieleza kuwa changamoto ya masomo kwa wanafunzi iliyopo,atatumia pesa atakayolipwa kuhakikisha wanafunzi wanapata vifaa vya kujifunza ili warudipo shuleni wawe vizuri kimasomo.
Kutokana na mauzo hayo ,watakaonufaika sio wakulima pekee bali hata vyama vya msingi kumi na tatu vitakavyopata Sh80milioni na halmashauri ya wilaya ya Urambo itakayojipatia Sh70milioni huku chama kikuu cha Milambo nacho kikitarajia kuingiza Sh34milioni.
Ununuzi wa tumbaku hiyo iliyobaki ambayo kutokana na kukaa muda mrefu ilianza kuharibika na nyingine kuingiliwa na wadudu,kunawapa unafuu wakulima ambao muda wowote mwezi huu wataanza kuuza tumbaku yao waliyovuna.



No comments:

Post a Comment