Featured Post

HALMASHAURI KALIUA YATOA MIKOPO SHILINGI MILIONI 240

MATANGAZO

Wednesday, December 1, 2021

HALMASHAURI KALIUA YATOA MIKOPO SHILINGI MILIONI 240


 Robert Kakwesi,Tabora

Tabora.   Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua,watu wake wamehamasika kwa kuunda vikundi vya  wajasiriamali 826 vyenye wanachama 8,820 ambavyo vinahitaji mikopo kutoka asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya makundi maalum ya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu.

Kutokana na hamasa kubwa iliyopekea idadi kubwa ya vikundi,mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo,Jerry Mwaga,anasema halmashauri inakabiliwa na changamoto kubwa kwani uwezo wake ni kutoa mikopo kwa vikundi 45 kwa mwaka.

Akizungumza wakati wa Utoaji Hundi yenye thamani ya Sh240milioni kwa vikundi vya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu 32,amesema sekta ya maendeleo ya Jamii ikutumika vizuri ,inaweza kuleta maendeleo Chanya na haraka kwa jamii.

"Fursa hii muhimu na adhimu ni lazima itumike vizuri kwa manufaa ya wahusika na jamii mzima kwa ujumla"Amesema

Mkurugenzi Mwaga pia amesema wanatoa hata vifaa kwa ajili ya wajasiriamali ambao 15 wamekabidhiwa pikipiki kwa ajili ya Biashara ya bodaboda huku watendaji 25 wakikabidhiwa pikipiki 25 kwa ajili ya utendaji kazi na kufanya zote 40 kuwa na thamani ya Sh69milioni.

Akikabidhi Hundi na pikipiki,mkuu wa mkoa wa Tabora,Dk Batilda Burian,amewahimiza wajasiriamali kurejesha mikopo kwa wakati ili na wengine na vikundi na wenyewe waweze kukopa.

Amewaasa kutofanya kiburi kwa kusubiri Hadi waanze kufuatwa au kutaka kupelekwa mahakamani ndio waanze kurejesha.

"Fursa hii mnayopata muitumie vizuri huku mkikumbuka na wengine wanasubiri mrejeshe ili nao wakope kamwe msisubiri mfuatwe au kutaka kupelekwa mahakamani ndio mrejeshe"Amesema.

Katika vikundi hivyo,vikundi  11 vya wanawake na vikundi 8 vya vijana ,vyote vikipata jumla ya Sh192milioni wakati vikundi 13 vya watu wenye ulemavu vikipata jumla ya Sh48milioni.


Tuesday, November 23, 2021

WILAYA YA KALIUA YAWAPUNGUZIA WAJAWAZITO KUJIFUNGULIA WILAYA JIRANI

 



Robert Kakwesi, Tabora

Hospitali ya Wilaya ya Kaliua,imehudumia wajawazito zaidi ya 300 katika kipindi Cha miezi kumi tangu kuanza kwake kutoa huduma.

 Katika kipindi hicho watoto zaidi ya mia tatu wamezaliwa huku wengine wakizaliwa kwa njia ya upasuaji.

 Tangu kuanzishwa kwake kuwa Wilaya mwaka 2014 ,Kaliua haikuwa na hospitali ya Wilaya baada ya kugawanywa iliyokuwa Wilaya ya Urambo na kuunda Wilaya mbili za Kaliua na Urambo.

 Kutokana na kutokuwa na hospitali yake ya Wilaya,wananchi wanaougua walikuwa wanalazimika kwenda Wilaya jirani za Uvinza,Urambo na Tabora umbali wa Hadi kufikia zaidi ya km120 na hivyo wagonjwa na wananchi kuteseka na kutumia kiasi kikubwa Cha fedha.

 Hata wajawazito nao wakilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma ya kujifungua na pale wanapolazimika kufanyiwa upasuaji Hali kuwa ngumu zaidi.

 Mganga mkuu wa halmashauri ya Wilaya ya Kaliua,Dk Lusubilo Adam,amesema wamehudumia kati ya wajawazito 300 Hadi 350 tangu waanze kutoa huduma.mwezi wa kumi mwaka Jana na kufanya zaidi ya wateja 700 kuhudumiwa wakiwemo wale wasiolazwa.

 "Mbali na kutoa huduma kwa wagonjwa na wajawazito,tumefanya upasuaji kwa wagonjwa wapatao hamsini na tunatoa huduma zilizo Bora"Amesema

 Dk Lusubilo ameongeza kuwa Wana wodi kubwa ya wajawazito inayoweza kuhudumiwa wajawazito 48 kwa wakati mmoja na kwamba dawa zipo na wataalamu wapo.

 Ameeleza kuwa wataanza kutoa huduma ya kulaza wanaume na watoto na pia huduma ya kuhifadhi maiti kwani majengo yake yamefikia hatua za mwisho kukamilika.

 Amesema kuanza kutoa huduma ya kulaza na kuhifadhi miili,kutawapunguzia gharama na muda wananchi waliokuwa wakifuata huduma wilaya jirani za Urambo na Tabora.

 Mmoja wa wanawake waliojifungua Hospitalini hapo,Zaituni Shaban,mkazi wa Ushokola,Amesema kwa kupata huduma hapo,wanaokoa fedha ambazo zinafanya shughuli zingine.

 "Tulikuwa tunapata shida ya kwenda Urambo na huko ndugu inabidi walale na kulazimika kutumia fedha nyingi tofauti na hapa"Amesema

 Mkazi wa Kazaroho,Mwanaidi Hassan,amesema mtoto wa jirani yake,alifariki baada ya kukosa huduma ya upasuaji kutokana na kukosa usafiri wa gari la kumkimbiza Wilaya Jirani ya Urambo.

 "Kama angepata usafiri Tena mapema,wangeweza kuokoa maisha yake ingawa kwa Sasa tunafurahi huduma ya upasuaji kufanyika hapa Kaliua"Amesema.

 Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Kaliua,Japhael Lufungija,amesema wameokoa muda na maisha ya watoto na wajawazito kwa kutolewa huduma wilayani Kaliua.

 Amesema baadhi ya watoto walikuwa wanapoteza maisha baada ya kuzaliwa kwa kukosa huduma muhimu ambazo hazikuwa zikitolewa kutokana na kukosekana hospitali ya Wilaya.

 Ameongeza kuwa wanaendelea kutenga bajeti ikiwa ni pamoja na kuomba Serikali Kuu ili majengo zaidi na madawa yapatikane na huduma ya mama na mtoto iwe nzuri zaidi.

 Wilaya ya Kaliua iliyoanzishwa mwaka 2014,haikuwa na Hospitali ya Wilaya na wakazi wake zaidi ya laki tatu,kutegemea huduma wilaya ya Urambo na Tabora umbali zaidi ya km 120.

 

Saturday, July 31, 2021

TABORA POLYTECHNIC YATARAJIA KUWA CHUO KIKUU HIVI KARIBUNI


 Robert Kakwesi, Tabora


Taasisi ya vyuo vya ufundi Tabora,Tabora Polytechnic college,kinatarajia kujipanua na kuwa Chuo Kikuu katika muda mfupi ujao.

Mkurugenzi wa Chuo hicho,Shaban Mrutu,alisema wanatambua hakuna Chuo Kikuu katika ukanda wa magharibi wenye mikoa ya Tabora,Katavi,Kigoma na Shinyanga na kuwa  kitakuwa Cha aina yake na mfano.

Akizungumza katika mahafali ya Saba ya Chuo hicho,alisema Chuo kina sifa zote za kupanuka na kuwa Chuo Kikuu ambacho kitatoa fursa kwa Wana Tabora na wakazi wa Kanda ya magharibi ,kunufaika na uwepo wa Chuo hicho kitakachotoa taaluma mbalimbali.

Mrutu pia alisema Wana mpango kuanzia baadae mwaka huu,kujenga hospitali katika Manispaa ya Tabora ambayo itasaidia kutoa huduma ya matibabu kwa wakazi wa Mkoa wa Tabora na hata nje ya mkoa.

"Tuna malengo makubwa ya kusaidia wakazi wa Tabora na mikoa jirani katika sekta za elimu na Afya"Amesema

Amebainisha kuwa wahitimu wa Chuo hicho,wanatoa wakiwa wameiva katika taaluma walizopata na kuwa jamii iwapokee na kuwapa Ushirikiano.

Alitamba kuwa Chuo hicho ni Bora,kikiwa na maabara kubwa na Vifaa vya kisasa yenye uwezo wa kuingiza wanafunzi 250 kwa wakati mmoja na kufanya majaribio.

Mrutu aliongeza kuwa Chuo hicho,kinazingatia Sana kupika wahitimu Bora na ndio maana kundi kubwa limeshindwa kumaliza katika fani mbalimbali.

Mwenyekiti wa bodi ya Chuo hicho,Lucas Ndanga,aliwataka wahitimu kutumia taaluma waliyopata kutoa huduma kwa jamii kwa weledi mkubwa na kujituma.

Ndanga ambaye ni wakili kitaaluma,Alisema muda waliokaa chuoni hapo umewajenga kupambana na maisha katika soko la ajira.

Mkuu wa Wilaya ya Tabora,Dk Yahaya Nawanda,mbali ya kukipongeza Chuo hicho,aliahidi kuwa anamzawadia mwanafunzi Bora Kila mwaka kiasi Cha shilingi laki mbili.

Pia aliahidi kuishawishi Manispaa ya Tabora,nayo kuunga mkono katika kumzawadia mwanafunzi Bora Kila mwaka wa Chuo hicho.


Wahitimu zaidi ya mia mbili na hamsini,wamehitimu katika Chuo hicho katika fani mbalimbali kama afisa tabibu,watunza kumbukumbu na wauguzi.

Monday, June 28, 2021

RC BATILDA ATOA SIKU 2 KUBORESHWA MACHINJIO


Machinjio ya nyama yaliyoko Mtaa wa Kariakoo katika halmashauri ya manispaa Tabora ambayo yanatakiwa kufanyiwa usafi wa kina ili kuboresha mazingira yake. Picha na Allan Ntana.


Na Allan Ntana, Tabora


MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya manispaa ya Tabora Bosco Ndunguru amepewa muda wa siku mbili kuhakikisha machinjio ya nyama yalioko eneo la Kariakoo yanafanyiwa usafi wa kina.


Agizo hilo limetolewa jana na Mkuu wa Mkoa huo Dkt Batilda Buriani alipotembelea na kukagua mazingura ya machinjio hayo akiambana na Mkuu wa wilaya na viongozi wa halmashauri ya manispaa hiyo.


Alisema hali ya usafi katika machinjio hayo hairidhishi, sakafu, kuta na mifereji ya kutolea uchafu ni vichafu sana na vyombo vya kuhifadhia nyama navyo haviridhishi ikiwemo uchakavu wa miundombinu.


Alisema lengo la kujengwa machinjio hayo ni kuongeza vyanzo vya mapato lakini kwa hali ilivyo sasa malengo hayo hayawezi kufikiwa tena hivyo akaagiza maboresho makubwa yafanyike ikiwemo kuanzisha vyanzo vingine vya mapato.


RC Batilda alimtaka Mkurugenzi kutoridhika na mapato wanayopata sasa bali wafanye kila linalowezekana ili kuhakikisha lengo la machinjio hayo kuwa kitovu cha kusafirisha nyama katika mataifa jirani ya Burundi na Rwanda linatimizwa.


‘Fanyeni usafi wa kina, nawapa siku 2 tu mandhari ya machinjio haya yabadilike, pakeni rangi kuta zote, wekeni marumaru (tiles) na maboksi yote ya kuwekea nyama yawe safi, sitaki mniangushe’, alisema RC.


Aliwataka kutumia sehemu ya mapato wanayokusanya kuboresha eneo hilo wakati wakisubiri mradi mkubwa wa Benki ya Dunia ambao utahusisha pia ujenzi wa machinjio hayo kwa kiwango cha kisasa.


Mkuu wa wilaya ya Tabora Mjini Dkt Yahaya Nawanda alimhakikishia kuwa atafanyia kazi maelekezo yote aliyoyatoa haraka iwezekanavyo ili kuhakikisha machinjio hayo yanakuwa na mwonekano mzuri ili kuongeza mapato.


Awali akitoa taarifa, Mkurugenzi Ndunguru alisema kuwa machinjio hayo yaliyojengwa kwa ufadhili wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Ulaya (European Economic Community) mwaka 1972 yanakabiliwa na changamoto kubwa ya uchakavu wa miundombinu hali inayosababisha usafi kutoridhisha.