Robert Kakwesi, Tabora
Hospitali ya Wilaya ya
Kaliua,imehudumia wajawazito zaidi ya 300 katika kipindi Cha miezi kumi tangu
kuanza kwake kutoa huduma.
Katika kipindi hicho watoto zaidi ya
mia tatu wamezaliwa huku wengine wakizaliwa kwa njia ya upasuaji.
Tangu kuanzishwa kwake kuwa Wilaya
mwaka 2014 ,Kaliua haikuwa na hospitali ya Wilaya baada ya kugawanywa iliyokuwa
Wilaya ya Urambo na kuunda Wilaya mbili za Kaliua na Urambo.
Kutokana na kutokuwa na hospitali
yake ya Wilaya,wananchi wanaougua walikuwa wanalazimika kwenda Wilaya jirani za
Uvinza,Urambo na Tabora umbali wa Hadi kufikia zaidi ya km120 na hivyo wagonjwa
na wananchi kuteseka na kutumia kiasi kikubwa Cha fedha.
Hata wajawazito nao wakilazimika
kusafiri umbali mrefu kufuata huduma ya kujifungua na pale wanapolazimika
kufanyiwa upasuaji Hali kuwa ngumu zaidi.
Mganga mkuu wa halmashauri ya Wilaya
ya Kaliua,Dk Lusubilo Adam,amesema wamehudumia kati ya wajawazito 300 Hadi 350
tangu waanze kutoa huduma.mwezi wa kumi mwaka Jana na kufanya zaidi ya wateja
700 kuhudumiwa wakiwemo wale wasiolazwa.
"Mbali na kutoa huduma kwa
wagonjwa na wajawazito,tumefanya upasuaji kwa wagonjwa wapatao hamsini na
tunatoa huduma zilizo Bora"Amesema
Dk Lusubilo ameongeza kuwa Wana wodi
kubwa ya wajawazito inayoweza kuhudumiwa wajawazito 48 kwa wakati mmoja na
kwamba dawa zipo na wataalamu wapo.
Ameeleza kuwa wataanza kutoa huduma
ya kulaza wanaume na watoto na pia huduma ya kuhifadhi maiti kwani majengo yake
yamefikia hatua za mwisho kukamilika.
Amesema kuanza kutoa huduma ya
kulaza na kuhifadhi miili,kutawapunguzia gharama na muda wananchi waliokuwa
wakifuata huduma wilaya jirani za Urambo na Tabora.
Mmoja wa wanawake waliojifungua
Hospitalini hapo,Zaituni Shaban,mkazi wa Ushokola,Amesema kwa kupata huduma
hapo,wanaokoa fedha ambazo zinafanya shughuli zingine.
"Tulikuwa tunapata shida ya
kwenda Urambo na huko ndugu inabidi walale na kulazimika kutumia fedha nyingi
tofauti na hapa"Amesema
Mkazi wa Kazaroho,Mwanaidi
Hassan,amesema mtoto wa jirani yake,alifariki baada ya kukosa huduma ya
upasuaji kutokana na kukosa usafiri wa gari la kumkimbiza Wilaya Jirani ya
Urambo.
"Kama angepata usafiri Tena
mapema,wangeweza kuokoa maisha yake ingawa kwa Sasa tunafurahi huduma ya
upasuaji kufanyika hapa Kaliua"Amesema.
Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya
ya Kaliua,Japhael Lufungija,amesema wameokoa muda na maisha ya watoto na
wajawazito kwa kutolewa huduma wilayani Kaliua.
Amesema baadhi ya watoto walikuwa
wanapoteza maisha baada ya kuzaliwa kwa kukosa huduma muhimu ambazo hazikuwa
zikitolewa kutokana na kukosekana hospitali ya Wilaya.
Ameongeza kuwa wanaendelea kutenga
bajeti ikiwa ni pamoja na kuomba Serikali Kuu ili majengo zaidi na madawa
yapatikane na huduma ya mama na mtoto iwe nzuri zaidi.
Wilaya ya Kaliua iliyoanzishwa mwaka
2014,haikuwa na Hospitali ya Wilaya na wakazi wake zaidi ya laki tatu,kutegemea
huduma wilaya ya Urambo na Tabora umbali zaidi ya km 120.
No comments:
Post a Comment