Featured Post

HALMASHAURI KALIUA YATOA MIKOPO SHILINGI MILIONI 240

MATANGAZO

Wednesday, March 24, 2021

KAMATI SIASA CCM TABORA YATETEA WAKANDARASI WAZAWA

 Robert Kakwesi, Tabora


Kamati ya siasa Mkoa wa Tabora,CCM, imeiomba Serikali kutoa kipaumbele kwa Wakandarasi wazawa katika eneo husika kwenye miradi ya ujenzi pindi inapotangazwa ili kuwaimarisha kimitaji na uwezo na kuimarisha uchumi wa eneo husika.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora kwa niaba ya Chama chake,Hassan Wakasuvi, wakati alipoongoza  wajumbe wenzake Kamati ya Siasa kukagua ujenzi wa  barabara ya Urambo hadi Kaliua,yenye urefu wa Km  28 iliyojengwa na Kampuni ya Samota..

Alisema Wakandarasi wazawa ambao wanaonyesha uwezo na uaminifu katika utekelezaji wa miradi ikiwemo ya ujenzi wa barabara pindi zabuni zinapotangazwa na wao kuomba, wapewe upendeleo kwa ajili ya kuwajenga na kuwaimarisha zaidi ili wakue na kuweza nao kuomba kazi nje ya Nchi.

Hatua hii itasaidia kupunguza gharama ya mradi kwa Serikali kwa kuwa Mkandarasi wa eneo husika hatakuwa na gharama kubwa za usafishaji wa mitambo kutoka mbali"Alisema

Mwenyekiti huyo alitoa wito kwa viongozi wa CCM kuanzia ngazi ya Shina hadi Mkoa na wananchi wote kuwa walinzi wa miundombinu inayojengwa kwa kuwafichua wezi wa alama za barabara ili iweze kuwa rafiki kwa watumiaji.

Alisema kung’oa  alama hizo kumekuwa kukirudisha nyuma juhudi kubwa za Serikali na kuongeza lazima wahalifu wafichuliwe na kuchukuliwa hatua kali ili kudhibiti uovu huo.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Samota,Salumu Abdallah aliishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwaamini wazawa na kuwapatia miradi ya ujenzi wa barabara kubwa ikiwemo wao ambao wanajenga barabara ya kutoka Urambo hadi Kaliua kwa gharama ya Sh38.7bilioni.

Alisema hatua hiyo imewasaidia sana kuwajengea uwezo na kupata ujuzi kutoka Mshauri Msimamizi ambapo hivi sasa wana uwezo wa kufanya kazi nyingine kubwa za ujenzi wa barabara kutokana mafunzo wanayopata.

Abdallah alisema ni vema Serikali inapokuwa na miradi ikaweka utaratibu wa kutenga miradi ambayo wazawa wanapaswa kujenga kwa kuwa wao hawana uwezo wa kushindana kwenye zabuni na Kampuni za nje ya Nchi kutokana na mitaji yao kuwa midogo ukilinganisha na wageni.

Meneja wa Mkoa wa Tabora wa Wakala wa Barabara Nchini ,Tanroads, Damian Ndabalinze, alisema barabara hiyo ya kutoka Urambo hadi Kaliua imekamilika kwa kiwango kikubwa zilizobaki ni kazi ndogo ndogo ambazo zinatarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi huu.

Alisema baadhi ya shughuli zilizobaki ni pamoja na mifereji ya maji ya mvua, kuweka alama za kuvuka watu, kuweka mawe yanayoonyesha umbali, na kuchora michoro ya usalama barabarani .

No comments:

Post a Comment