Robert Kakwesi, Tabora
Taasisi ya vyuo vya ufundi Tabora,Tabora Polytechnic college,kinatarajia kujipanua na kuwa Chuo Kikuu katika muda mfupi ujao.
Mkurugenzi wa Chuo hicho,Shaban Mrutu,alisema wanatambua hakuna Chuo Kikuu katika ukanda wa magharibi wenye mikoa ya Tabora,Katavi,Kigoma na Shinyanga na kuwa kitakuwa Cha aina yake na mfano.
Akizungumza katika mahafali ya Saba ya Chuo hicho,alisema Chuo kina sifa zote za kupanuka na kuwa Chuo Kikuu ambacho kitatoa fursa kwa Wana Tabora na wakazi wa Kanda ya magharibi ,kunufaika na uwepo wa Chuo hicho kitakachotoa taaluma mbalimbali.
Mrutu pia alisema Wana mpango kuanzia baadae mwaka huu,kujenga hospitali katika Manispaa ya Tabora ambayo itasaidia kutoa huduma ya matibabu kwa wakazi wa Mkoa wa Tabora na hata nje ya mkoa.
"Tuna malengo makubwa ya kusaidia wakazi wa Tabora na mikoa jirani katika sekta za elimu na Afya"Amesema
Amebainisha kuwa wahitimu wa Chuo hicho,wanatoa wakiwa wameiva katika taaluma walizopata na kuwa jamii iwapokee na kuwapa Ushirikiano.
Alitamba kuwa Chuo hicho ni Bora,kikiwa na maabara kubwa na Vifaa vya kisasa yenye uwezo wa kuingiza wanafunzi 250 kwa wakati mmoja na kufanya majaribio.
Mrutu aliongeza kuwa Chuo hicho,kinazingatia Sana kupika wahitimu Bora na ndio maana kundi kubwa limeshindwa kumaliza katika fani mbalimbali.
Mwenyekiti wa bodi ya Chuo hicho,Lucas Ndanga,aliwataka wahitimu kutumia taaluma waliyopata kutoa huduma kwa jamii kwa weledi mkubwa na kujituma.
Ndanga ambaye ni wakili kitaaluma,Alisema muda waliokaa chuoni hapo umewajenga kupambana na maisha katika soko la ajira.
Mkuu wa Wilaya ya Tabora,Dk Yahaya Nawanda,mbali ya kukipongeza Chuo hicho,aliahidi kuwa anamzawadia mwanafunzi Bora Kila mwaka kiasi Cha shilingi laki mbili.
Pia aliahidi kuishawishi Manispaa ya Tabora,nayo kuunga mkono katika kumzawadia mwanafunzi Bora Kila mwaka wa Chuo hicho.
Wahitimu zaidi ya mia mbili na hamsini,wamehitimu katika Chuo hicho katika fani mbalimbali kama afisa tabibu,watunza kumbukumbu na wauguzi.